Mweka kuwa kitovu cha mafunzo, urithi wa dunia Afrika

Moshi. Wakati Tanzania ikiendelea kuweka mikakati ya kurejesha mali kale zilizoondolewa nchini wakati na baada ya utawala wa kikoloni, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kimeanzisha programu maalumu inayolenga kuzijengea uwezo nchi za Afrika katika kutambua, kuhifadhi na kulinda urithi wa asili na wa kitamaduni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo leo, Agosti 26,2025 Naibu Mkuu wa Chuo cha Mweka, Dk Alex Kisingo amesema kuwa mradi huo utatoa fursa kwa Tanzania, Afrika Kusini, Senegal, Cameroon, na Morocco, huku chuo hicho kikitarajiwa kuwa kitovu cha umahiri katika utoaji wa elimu ya utambuzi na ulinzi wa urithi wa dunia.

“Katika mradi huu tutakuwa na mitaala maalumu ya usimamizi wa maeneo ya urithi wa dunia, sambamba na programu zitakazowafundisha watu namna ya kuyatumia maeneo hayo kwa njia za kiuchumi,” amesema Dk Kisingo.

Dk Kisingo amesema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), na unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu, na  wanafunzi kutoka nchi mbalimbali watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho.

“Mradi huu ni fursa adhimu kwa Tanzania kushirikiana na mataifa mengine manne ya Afrika katika kuandaa mitaala na kuendeleza vituo vya umahiri vya kutoa elimu ya utambuzi na ulinzi wa urithi wa kitamaduni na wa asili,”amesema Dk Kisingo

Amesema; “Hii ni heshima kubwa kwa taasisi yetu na kwa Taifa kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na urithi wa kipekee unaoweza kutumika kama chachu ya maendeleo ya wananchi wetu.”

Dk Kisingo, amesema programu hiyo pia inalenga kuibua maeneo mapya ya urithi ambayo yanaweza kubadilishwa kuwa vivutio vya utalii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

Naye, Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje (Stesheni ya Arusha), Assah Mwambene amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi vinara duniani katika kuzalisha wataalamu wa kutambua na kutunza mali kale zinazotambuliwa na Unesco.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa ‘Africa Unite’ kutoka Unesco, Rouran Zhang amesema kuwa bara la Afrika lina urithi wa kipekee wa kitamaduni na wa asili, lakini bado haujaakisiwa vya kutosha kwenye orodha ya urithi wa dunia.

“Tunaamini kuwa suluhisho la kweli linapaswa kutoka barani Afrika lenyewe na liwe endelevu. Tunaona mwelekeo huo kupitia vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ambazo zinawaandaa wataalamu wa kizazi kijacho, kuzalisha maarifa yanayoendana na muktadha wa Kiafrika, na kutoa huduma za kiufundi kwa nchi wanachama pamoja na wasimamizi wa maeneo ya urithi,” amesema  Zhang.