Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Zanzibar imepiga hatua katika masuala ya usawa wa kijinsia kuanzia kwenye sera na sheria zilizopo.
Amesema Serikali imeanza utekelezaji wake kuhakikisha usalama wa wanawake unazingatiwa kwa kuweka miundombinu bora kwao.
Dk Mwinyi ameeleza hayo leo Jumanne Agosti 26, 2025 katika ufunguzi wa mkutano wa saba wa dunia wa miji na maeneo salama ya kijamii kwa wanawake, uliofanyika Mjini Unguja.
Amesema mambo mawili ndio yamechangia Zanzibar kupiga hatua katika suala la usawa wa kijinsia ikiwemo kutunga sera nzuri na sheria na kuhakikisha zinatekelezwa.
“Zanzibar ukiacha kuwa na sera nzuri tumezitungia sheria na kuhakikisha zinasimamiwa ipasavyo katika utekelezaji wake kwa kuimarisha ulinzi na usalama,” amesema Dk Mwinyi.

Viongozi mbalimbali walioshiriki katika ufunguzi wa mkutano wa saba wa unaohusu miji na maeneo salama ya umma kwa wanawake uliofanyika Mjini Unguja.
Ameeleza kufanyika kwa mkutano huo kisiwani humo ni dhahiri kuwa wametambua juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kutoa kipaumbele zaidi katika suala hilo.
Amebainisha kuwa licha ya Zanzibar kupiga hatua katika eneo la usawa wa kijinsia, mkutano huo utasaidia kupata mbinu mpya kutoka kwa viongozi wa nchi nyingine kwa kubadilishana ujuzi na kuona namna ya kuboresha.
Pia, Rais Mwinyi amesema Serikali ina mikakati mingi ya kuondoa unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia, kwa kuwawezesha makundi ya wanawake mbalimbali kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ya kufanyia kazi.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mussa amesema Zanzibar inajivunia kuwa kuiunganishi cha jadi na mageuzi ya jamii kwa kugeuza maadili ya pamoja.
Amesema mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya kutengeneza urafiki wa kudumu na Zanzibar inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Wanawake (UN Women).
Amefafanua kuwa watatumia mkutano huo kutafsiri maono ya miji salama na kuyaweka katika utekelezaji, kwani usalama wa umma ndio heshima na msingi wa kibinadamu kwa maendeleo endelevu.
“Kupiga hatua katika safari hii kunahitaji uongozi thabiti na wenye maono na kuonyesha alama kwa kuweka usawa na usalama wa ustawi wa jamii,” amesema Mahmoud.
Naye Mkuu wa Uchumi na Utawala kutoka wa UN Women, Dorota Paneyzyk amesema usawa wa kijinsia sio tu kupata haki, badala ya kuwa katika maeneo salama kwa lengo la kufikia fursa za maendeleo yao ya baadaye.
Waziri wa Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma amesema usimamizi wa usawa kisiwani humo unazingatiwa kupitia sera na sheria zilizopo ambazo zinasaidia kufikia malengo yao.