Shule zisaidie kufundisha watoto uzalendo

Dar es Salaam. Uzalendo ni moyo wa kuipenda nchi yako, kuithamini, na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa lako.

Ni thamani inayojengwa na kuendelezwa kwa makusudi, si jambo la kimaumbile tu. Katika hali ya sasa ambapo taifa linakumbwa na changamoto nyingi za kimaadili, kiuchumi na kijamii, ipo haja ya dharura ya kujenga kizazi kipya chenye moyo wa uzalendo wa kweli.

Kwa nionavyo mimi, mahala  pa kuanzia katika ujenzi wa  kazi hii adhimu si pengine zaidi ya shuleni. Shule zina nafasi ya kipekee ya kuwajengea watoto maadili na misingi ya kuipenda nchi yao tangu wakiwa wadogo.

Kwa miaka mingi, tumeshuhudia ongezeko la viongozi wa umma na wanasiasa wanaotanguliza maslahi yao binafsi badala ya yale ya wananchi waliowachagua. Watumishi wa umma, ambao walipaswa kuwa mifano bora ya uzalendo kwa kutoa huduma bora kwa wananchi, wamegeuka kuwa chanzo cha matatizo kwa kutojali wajibu wao, kuchelewesha huduma, na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mtu anayejali kweli nchi yake hawezi kushiriki kwa namna yoyote ile katika kuiumiza. Lakini ukweli mchungu ni kwamba, sehemu kubwa ya watumishi wa Serikali leo hawajali kuhusu athari ya uzembe wao kwa taifa kwa ujumla.

Katika ofisi nyingi za umma, wananchi husubiri kwa saa kadhaa bila kuhudumiwa kwa wakati. Kuna tabia ya baadhi ya watumishi kuchelewa kazini, kutoka mapema, au hata kuwapuuza wananchi wanaohitaji msaada.

Wanapokosolewa, hutoa visingizio badala ya kujirekebisha. Wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kutumia ofisi za umma kujinufaisha binafsi kupitia mianya ya kifisadi.

Hii yote ni ishara ya ukosefu wa uzalendo. Mtu mwenye uzalendo hawezi kutumia nafasi yake kuiibia nchi, kuichelewesha, au kuikwamisha katika maendeleo.

Kwa upande wa viongozi wa kisiasa, hali ni ya kusikitisha zaidi. Wengi wao wanapoingia madarakani husahau ahadi walizotoa kwa wananchi. Badala ya kushughulika na matatizo ya umma kama elimu, afya, miundombinu, au ajira kwa vijana, hujikita katika kuongeza vipato vyao binafsi, kuhudhuria mikutano ya kifahari, au kupigania posho na marupurupu yasiyo na tija kwa mwananchi wa kawaida.

Wengine huongeza mivutano ya kisiasa,  chuki  na hata kususia shughuli za kisiasa za taifa badala ya kuhimiza mshikamano wa kitaifa. Hii yote ni ishara tosha kwamba uzalendo umepotea au haukufundishwa ipasavyo katika maisha yao ya awali.

Uzalendo hauanzi kwenye siasa wala ofisi za Serikali. Uzalendo hujengwa tangu utotoni. Na shule ni uwanja muhimu wa kazi hii.

Mtoto anayefundishwa kupenda taifa lake, kuheshimu rasilimali za nchi, kujitolea kwa ajili ya wengine, na kuwa na maadili ya kitaifa, hukua akiwa mtu mwenye moyo wa kuchangia maendeleo ya taifa lake bila shuruti.

Lakini hali ya sasa inaonyesha kwamba masuala ya uzalendo bado hayajapewa uzito katika mitalaa yetu ya elimu. Mara nyingi, elimu imejikita katika namba, vyeti, na ufaulu wa mitihani ya darasani, badala ya malezi ya tabia na maadili ya kitaifa.

Shule zetu zinapaswa kuwa sehemu ya kwanza ya kufundisha uzalendo kwa vitendo. Walimu wawe wa kwanza kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwahi kazini, kuwaheshimu wanafunzi, kufanya kazi kwa bidii, na kuwahimiza watoto kuipenda nchi yao kwa maneno na matendo.

Masomo ya historia, uraia, na maarifa ya jamii yafundishwe  kivitendo zaidi na  kuonyesha matukio muhimu ya kitaifa, historia ya mashujaa wa taifa, na thamani ya kulinda amani na umoja.

Watoto wafundishwe pia umuhimu wa kulipa kodi, kutunza mazingira, kulinda miundombinu ya umma kama shule na hospitali na kusema ukweli.

Zaidi ya hayo, shule zianzishe programu za vitendo zinazolenga kuhimiza uzalendo. Hizi ni pamoja na shughuli za usafi wa jamii, kampeni za upandaji miti, kutembelea maeneo ya kihistoria ya kitaifa, kushiriki matamasha ya kumbukumbu za kitaifa, na kujifunza wimbo wa taifa kwa maana yake ya kina.

Shughuli hizi si tu zinawafundisha watoto kushiriki katika maendeleo ya jamii, bali zinawajengea hisia ya kuwa sehemu ya Taifa.

Mtoto anayejifunza kuilinda rangi ya bendera yake, kusherehekea uhuru wa nchi yake, na kujivunia lugha na tamaduni zake, hawezi kuwa fisadi au mzembe anapokua.

Pia kuna haja ya kuboresha maudhui ya mitalaa ili kuingiza dhana za  uzalendo si kwa nadharia pekee, bali kwa mafunzo ya kina yanayogusa maisha halisi.

Watoto wafundishwe kuhusu majukumu ya raia, namna ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa, na sababu za kupinga rushwa, ukabila, udini na chuki za kisiasa.

Shule zishirikiane na taasisi mbalimbali za kijamii, kijeshi, na za kihistoria kuandaa semina au warsha za kuwajengea wanafunzi uelewa mpana.

Natambua uzalendo umepewa msukumo katika mtalaa ulioboreshwa. Hilo ni jambo jema, lakini je, ufundishwaji wake ni wa vitendo au ule wa kumaliza chaki na kujaza kurasa za madaftari?

Natamani kuona watoto wakipelekwa mitaani,  kwenye taasisi za umma kama hospitali na maeneo mengine wakijifunza  kivitendo mambo  mbalimbali yanayoweza kukuza uzalendo kwa Taifa lao.