WINGA wa zamani wa Azam FC, Gibril Sillah ameshindwa kujizuia na kummwagia sifa nyota wa timu hiyo, Tepsie Evans akisema makali na kipaji kikubwa alichonacho kitakuwa msaada mkubwa kwa kikosi hicho baada ya kuondoka kwake.
Azam chini ya kocha Florent Ibenge imekita kambi jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na imecheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya AS Kigali ikipoteza kwa kufungwa bao 1-1, sare ya 1-1 dhidi ya Police FC na ile ya tatu ikashinda 2-0 dhidi ya APR.
Sillah ambaye alikitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili akitokea Raja Casablanca ya Morocco akicheza mechi 68 akafunga mabao 21 na asisti 10, alisema baada ya kuondoka amemwachia kijiti Tepsie ambaye anaamini atafiti eneo hilo.
Msimu uliopita Tepsie hakuanza vizuri alipojiunga tena na Azam dirisha dogo akitokea KMC kwa mkopo baada ya kupata jeraha la mguu.
“Ni muda sasa wa Tepsie kuwaonyesha Tanzania wewe ni nani… kipaji kikubwa sana na nimekuachia kijiti uendelee nacho,” aliandika Sillah kwenye posti ya Tepsie mtandaoni.
Eneo analocheza Tepsie wapo nyota Lamine Jorjou aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Al Hilal ya Sudan, Zidane Sereri, Idd Nado na Abdul Suleiman ‘Sopu’. Azam inajiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuvaana na El Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini na kama itapenya raundi ya kwanza itavaana na mshindi kati ya KMKM na AS Port ya Djibouti.