Trump atangaza adhabu kali wanaodhalilisha bendera ya Marekani

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini amri ya kiutendaji (Executive Order), inayopiga marufuku kitendo cha kuchoma bendera ya nchi hiyo, akisema yeyote atakayefanya hivyo atakwenda jela mwaka mmoja bila msamaha.

Kwa mujibu wa CBS News, Al Jazeera na tovuti rasmi ya The White House wanaochoma bendera watafungwa mwaka mmoja na kuwekewa rekodi ya jinai.

Mwanasheria mkuu ameagizwa kuhakikisha kesi hizo zinashtakiwa kwa kiwango cha juu kabisa. Pia, kwa wageni watakaochoma bendera watapata adhabu ikiwemo kufutiwa viza na kufukuzwa nchini humo.

Tovuti ya The White House imesema hati hiyo ya amri ya rais iliyotiwa saini na Trump jana Jumatatu, Agosti 25, 2025 inataka kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya vitendo hivyo vya kuchoma au kudhalilisha bendera ya Marekani.

Kwa ufupi, amri hiyo inamaanisha bendera ya Marekani inaelezwa kama alama takatifu ya taifa, uhuru na mshikamano wa Wamarekani.

Sasa kitendo cha kuichoma au kuidhalilisha kinachukuliwa kama cha dharau na chenye kuhamasisha vurugu.

Ingawa Mahakama kuu imetambua kuchoma bendera kama sehemu ya uhuru wa kujieleza (katika kesi Texas v. Johnson, 1989), amri hii inalenga kuzidisha utekelezaji pale ambapo kitendo hicho kinasababisha vurugu, uchochezi wa uhalifu, au kinahesabika kama “fighting words.”

Mwanasheria mkuu wa serikali atapewa kipaumbele cha kisheria kushughulikia kesi za kudhalilishwa kwa bendera pale ambapo zinakiuka sheria zilizopo (kama uharibifu wa mali, uchochezi, vurugu, au uhalifu wa chuki).

Ikiwa kitendo kinakiuka sheria za majimbo au serikali za mitaa (mfano: sheria za kuchoma hadharani, kuvuruga amani, au uharibifu wa mali), kesi itapelekwa kwa mamlaka husika za ndani.

Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara ya Uhamiaji zitafuta viza, kibali cha ukaazi, uraia, au kuamuru kufukuzwa nchini kwa wageni waliodhalilisha bendera chini ya masharti ya sheria za Marekani.

Kwa kifupi, amri hii inalenga kupanua ufuatiliaji na adhabu kwa vitendo vya kudhalilisha bendera ya Marekani, hasa pale ambapo vinaambatana na uchochezi wa vurugu, uhalifu, au vitisho, huku ikilenga pia kuwabana wageni wanaofanya vitendo hivyo.

Hata hivyo, CBS News imeripoti makundi ya utetezi wa uhuru wa kujieleza  yamesema hatua ya Trump ni kinyume na Katiba na haiwezi kufutwa kwa “kalamu ya Rais”.

Wanasheria wameeleza hakuna ushahidi kwamba kuchoma bendera kumesababisha ghasia kubwa au tishio la kitaifa.

Profesa GS Hans wa Chuo Kikuu cha Cornell amesema ni “suluhisho linalotafuta tatizo,” akimaanisha halina msingi wa kisheria wala kijamii.