Vodacom kuwapa kipaumbele zaidi watu ushirikiano ESG

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuweka watu mbele katika utekelezaji wa ushirikiano wake wa mfumo wa Mazingira, Jamii, na Utawala Bora (ESG).

Hayo yamebainishwa leo Jumanne, Agosti 26, 2025 kwenye uzinduzi wa mfumo jumuishi wa Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG) wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL).

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje kutoka Vodacom Tanzania, Zuweina Farah amesema msingi wa ushirikiano wowote ni kuendana kwa mikakati ya pande zote.

“Vodacom inalenga kusaidia jamii mbalimbali kwa kujumuisha na kujiandaa na majanga, kutoa msaada wa dharura, na kujitokeza pale jamii zinapohitaji msaada.
“Kulinda sayari ambapo suala hili linafanikishwa kupitia mipango inayojali mazingira. Pamoja na kudumisha uaminifu kwa kuhakikisha wateja wanapata ulinzi wa data na usalama mtandaoni,” amesema. 

Kulingana na Farah, Vodacom inatambua kuwa uunganishaji wa kidijitali (connectivity) ni muhimu ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata ulimwengu wa kidijitali.
Zaidi ya hayo, kampuni inalinda wateja wake kupitia kampeni za uhamasishaji kuhusu ulaghai, ulinzi wa data, na usalama wa mitandao.

Amesema mwisho wa yote lengo kuu la kampuni ni jinsi mradi unavyoweza kubadilisha maisha ya watu na kuongeza thamani ya kudumu.