Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kulia), akikata utepe kuzindua Ripoti ya ESG yenye kaulimbiu “Connecting for Good: People, Planet and Possibilities”, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire. Ripoti hiyo inaonesha mchango wa teknolojia na huduma za mawasiliano katika kubadilisha maisha ya watu, kuongeza ujumuishwaji wa kijamii pamoja na kuchochea maendeleo endelevu yanayozingatia mazingira, jamii na misingi ya utawala bora. Uzinduzi huo umefanyika Agosti 26 jijini Dar es Salaam.
Vodacom Tanzania imezindua rasmi ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) chini ya kaulimbiu “Connecting for Good: People, Planet and Possibilities.”
Ripoti hii inaonyesha jinsi huduma za mawasiliano zinavyobadilisha maisha ya wananchi, kukuza ujumuishwaji wa jamii na kuchochea maendeleo endelevu nchini.
Uzinduzi wa ripoti hiyo umefanyika leo jijini Dar es Salaam ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire.
Prof. Mkumbo amezitaka sekta binafsi na serikali kuimarisha ushirikiano, “Kawaida, serikali inaonekana kama mkusanyaji kodi na sekta binafsi kama mlipa kodi. Tunapaswa kuangalia zaidi ya hapo na kutambua kila upande kama mshirika muhimu katika maendeleo ya taifa. Ushirikiano halisi unapaswa kuleta matokeo chanya,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisisitiza umuhimu wa huduma za mawasiliano katika kuleta mabadiliko chanya “Ripoti hii ya ESG inaonesha dhamira yetu kwa wananchi wa Tanzania. Mawasiliano siyo tu kuhusu minara na nyaya, ni kuhusu kuunda fursa, kuwezesha jamii na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” alisema.
Ripoti hiyo pia inaangazia uwekezaji wa Vodacom kuwekeza katika bunifu mbali mbali ili kuwawezesha watanzania kutumia huduma za kidijitali, ujumuishi wa kifedha, uwezeshaji wa vijana na utunzaji wa mazingira, sambamba na Maono ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Uzinduzi huo, ulioratibiwa kwa kushirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL), ulihudhuriwa na wadau kutoka sekta za serikali, binafsi na asasi mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya uwajibikaji na biashara yenye dhamira.