Dar es Salaam. Raia wa Ghana, Valentine Kofi (45) na Watanzania watatu, wataendelea kubaki rumande hadi Septemba 8, 2025 wakati kesi yao ya uhujumu uchumi itakapotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika. Kofi na wenzake wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2 bilioni, mali ya benki ya Banc ABC.
Leo Jumanne Agosti 26, 2025 Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Pia, upande wa mashtaka umedai tarehe ijayo watafanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kuongeza mshtakiwa mwingine.
Hakimu Mhini alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 8, 2025.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutoka na shtaka la kitakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Kofi ambaye ni mkazi ya Mikocheni washtakiwa wengine ni Patrick Tarimo(34) mkazi wa Kibaha, Aisha Kagashe(40) mkazi wa Sinza na Idan Msuya(46) mkazi wa Mikocheni.
Kwa mujibu wa kesi ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Septemba Mosi, 2021 na Oktoba 25, 2021 ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi tisa za Afrika ambazo ni Ghana, Ivory Coast, Uganda, Zambia, Senegal, Cameroon, Ufaransa, Mali na Bukinafaso.
Inadaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliongoza genge hilo kwa kuingilia mfumo wa benki ya African Banking Corporation of Tanzania Limited (Banc ABC) kwa lengo la kuiba Sh2 bilioni mali ya benki hiyo.
Shtaka la pili ni kuingilia mfumo wa benki, ambapo washtakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani siku na maeneo hayo, waliingilia mfumo wa kompyuta wa benki hiyo na kudukua akaunti 160 za visa za malipo ya awali zilizopo katika benki hiyo na kupelekea benki hiyo ipate deni la Sh3.5 bilioni.
Shtaka la tatu ni wizi, tukio wanalodaiwa kulitenda Oktoba 24 na Oktoba 25, 2021 katika maeneo hayo, ambapo washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliiba Sh2 bilioni kupitia kadi ya viza ya malipo ya awali kutoka katika benki hiyo.
Shtaka la nne ni kutakatisha fedha, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 24, 2021 na Februari 18, 2025 katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi hizo, washtakiwa kwa pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, walijipatia Sh2 bilioni mali ya benki hiyo wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la wizi.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 13, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.