DROO ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake kutoka Ukanda wa Afrika Masharikia na Kati (Cecafa) inatarajiwa kuchezeshwa leo Nairobi, Kenya ambapo wapinzani wa wawakilishi wa Tanzania, JKT Queens, watafahamika.
Ratiba inaonyesha michuano hiyo itaanza kuchezwa kati ya Septemba 4-16 kwenye viwanja vya Nyayo na Ulinzi Complex nchini humo.
Kwa mujibu wa meneja wa Mashindano wa Cecafa, Yusuf Mossi mechi za kufuzu zitashirikisha timu tisa ikiwemo JKT Queens ya Tanzania, Rayon Sports Women (Rwanda), Kampala Queens (Uganda) na CBE (Ethiopia).
Timu nyingine ni Kenya Police Bullets (Kenya), The Joint Stars (Sudan Kusini), JKU Princess (Zanzibar), Top Girls Academy (Burundi) na Denden (Eritrea).
JKT Queens itaiwakilisha Tanzania baada ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu uliopita na hii ni mara ya pili kwa timu hiyo kushirikia, kwani ilishiriki 2023 na kubeba taji la michuano hiyo kwa kuifunga C.B.E kwa mikwaju ya penalti 5-4 kufuatia sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida wa mechi.
Hii inakuwa mara ya tano kwa Tanzania kupeleka timu katika michuano hiyo tangu ilipoasisiwa 2021, ambapo awali Simba Queens ilishiriki 2021 ikatolewa nusu fainali na Vihiga Queens ya Kenya kwa mabao 2-1. Mwaka uliofuata ilishiriki tena ikanyakua ubingwa mbele ya She Cooperate ya Uganda kwa kuichapa bao 1-0 na kwenda kuiwakilisha Cecafa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mwaka 2023 JKT ikashiriki kwa mara ya kwanza mashindano yaliyofanyika Uganda na maafande hao wakanyakua ubingwa huo mbele ya C.B.E ya Ethiopia na kukata tiketi ya CAF ambapo hata hivyo, haikufanya vizuri kwani iliishia makundi.
Msimu uliopita Simba kwa mara nyingine ilishiriki na kuishia nusu fainali kwa kuifumuliwa mabao 3-2 na Polisi Kenya na sasa ni zamu ya maafande wa JKT Queens.