Gaza. Watu 21 wameuawa kufuatia shambulizi la bomu lililopigwa na Israel kwenye hospitali ya Nasser kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Al Jazeera imeripoti kuwa miongoni mwa waliouawa ni waandishi wa habari watano waliokuwa wakifanya kazi katika mashirika ya Al Jazeera, Reuters na ya Associated Press (AP).
Wengine ni madaktari na waokoaji, waliokuwa wakifanya kazi katika hospitali hiyo ambayo imekuwa kimbilio kwa wakazi wa mji huo kufuatia mapigano yanayoendelea.
Shambulizi hilo linakuja wakati Israel ikiwa inaendelea kupanua mashambulizi yake kwenye maeneo yenye wakazi wengi na vituo vya mijini, ikiwa ni pamoja na Jiji la Gaza, na kuongeza hatari ambayo tayari imeongezeka kwa idadi ya watu.
Akielezea tukio hilo daktari wa kitengo cha watoto hospitalini hapo, Dk Ahmed al-Farra amesema bomu hilo lilipigwa mara mbili likigonga ukuta wa ghorofa la hospitali hiyo kabla ya waandishi na waokoaji waliokuwa chini kuanza kupanda juu.
Amesema baada ya shambulizi hilo, waandishi na waokoaji walianza kupanda juu kwa kutumia ngazi za nje ya jengo hilo wakiwa wamevalia fulana za rangi ya chungwa.
“Shambulio hili limeathiri wapita njia na watu wanaoishi karibu na hospitali, pamoja na wagonjwa ambao wanapokea matibabu katika mojawapo ya maeneo haya, ambayo yanahitaji ulinzi chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu,” amesema Dk Ahmed.
Dk Ahmed ameomba kuchukuliwa kwa hatua za kukomesha mauaji hayo na kuweka vizuizi kwenye matumizi ya silaha.

Baada ya shambulizi hilo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Misaada ya Kibinadamu (OCHA) ilitoa wito mpya wa kupelekwa kwa misaada ndani ya ukanda wa Gaza ili kuondoa hatari ya vifo vinavyotokana na njaa.
Ofisi hiyo imesema hali ya njaa imethibitishwa kuwa kubwa kwa sasa katika eneo lote la Gaza na kuongezeka kwa utapiamlo miongoni mwa watoto ambao ni waathirika wa janga la njaa linalotokana na vita hivi.
“Ni vigumu kutotumia sifa za juu zaidi katika muktadha huu, lakini kwa kweli, hili ni janga la kipekee kwa binadamu na janga baya zaidi ambalo limewahi kushuhudiwa,” imeeleza ofisi hiyo.
Shambulizi hilo linaongeza idadi ya vifo vya waandishi wa habari wa Kipalestina waliouawa huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023 kufikikia 273, kwa mujibu wa hesabu ya Al Jazeera.
Kamati ya kulinda waandishi wa habari imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuiwajibisha Israel kwa kuendelea kushambulia vyombo vya habari kinyume cha sheria.
Imeandikwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa mashirika ya habari.