Afrika Kusini kupigania msaada mapambano ya Ukimwi

Pretoria. Serikali ya Afrika Kusini imesema haitaruhusu kuondolewa kwa takribani (dola milioni 427) sawa na Sh1.1 trilioni zilizokuwa zinatolewa na Marekani, kudhoofisha programu yake kubwa ya kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Kwa mujibu wa AP News, Programu hiyo, ingawa ni kubwa inakabiliana na changamoto, huku wataalamu wa afya wakionya kuwa katika miaka michache ijayo, nchi inaweza kushuhudia maambukizi mapya ya maelfu ya watu.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi duniani. Hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kupunguza bajeti ya msaada wa kigeni ilileta athari mara moja, kliniki nyingi za bure ziligoma kutoa huduma, na wagonjwa wengi kuachwa bila dawa.

Baadhi ya waanzilishi wa kikundi cha Advocary for Prevention of HIV and AIDs, nchini humo, Yvette Raphael amesema hali ya hofu itaendelea kama Serikali haitafanya mchakato wa kupambana dhidi ya ugonjwa huo.

“Tunawaogopa kwamba tutashuhudia idadi kubwa ya watu wanaoishi na HIV ikiongezeka. Tuna wasiwasi kuhusu idadi ya watoto watakaozaliwa na maambukizi kutokana na upungufu wa huduma. Pesa tulizokuwa tukipokea kutoka USAid zilikuwa zikifunika pengo ambalo Serikali yetu haikuweza kulitatua,” amesema Raphael.

Hata kabla ya kupunguzwa kwa msaada, kati ya watu takriban milioni nane waliokuwa na maambukizi nchini humo, watu milioni mbili tu ndio walikuwa wanapokea dawa.

Hofu ya kuongezeka kwa maambukizi

Baadhi ya watu waliokuwa wanachukua dawa kwenye vituo mbalimbali wamesema msaada wa kifedha ulikokuwa ukitolewa na Marekani ulikuwa muhimu sana maishani mwao. 

“Maisha yetu ni muhimu, sisi ni binadamu, zile kliniki zilikuwa muhimu kwetu kwa matibabu. Msaada wa kifedha ulikuwa muhimu maishani mwetu. Kliniki ingekuja katika nyumba yangu, ikinipa huduma pale. Ingeniangalia kila baada ya miezi mitatu na kunipa dawa,” amesema mgonjwa ambaye hakutaka jina lake kutajwa.

Akinukuliwa na AP News ameongeza kwa kusema, “Nilihitaji tu kuenda kliniki kwa ajili dawa pia, kila nilipohitaji kondomu au vilainishi ilikuwa inanipatia.”

Hali hiyo inazidi kuathiri Afrika kwa ujumla, bara lililoathirika na kupunguzwa kwa msaada wa Marekani. Serikali ya Trump ilijitetea kwa kusema matumizi hayo hayakuendana na masilahi ya Marekani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ofisi ya Usimamizi wa Bajeti ya Marekani, Russel Vougt kwenye kikao cha ushauri Juni mwaka huu alisema, “Tuna deni la (dola trilioni 37) sawa na Sh93 trilioni. Hivyo basi, wakati fulani, bara la Afrika linapaswa kubeba zaidi ya mzigo wa kutoa huduma hizi za afya.”

Baadhi ya raia wa Afrika Kusini wanasema msimamo wa Trump unaweza kuathiriwa na Mmarekani wa asili ya nchi hiyo, Elon Musk, ambaye alihusishwa na juhudi za awali za kupunguza msaada wa Marekani.

Marekani imeidhinisha marekebisho madogo ili baadhi ya huduma muhimu za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi ziendelee, lakini upungufu wa msaada umeleta pengo. Kwa wengi waliokumbwa na kupunguzwa kwa msaada, madhara tayari yameonekana.

Imeandikwa na Mintanga Hunda kwa msaada wa mtandao.