Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyokaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu dereva bodaboda, Ibrahim Othman maarufu kama Boban, kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.
Othman, anadaiwa kumuua dereva bodababoda mwenzake, aitwaye Mahmud Peya, tukio analodaiwa kulitenda Februari 4, 2023, Mbagala Kuu njia ya Chang’ombe, Wilaya ya Temeke.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo akishirikiana na wenzake ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, baada ya kumkodi dereva huyo na kisha kumuua na kuiba pikipiki aina ya Boxer, ambayo baadaye aliipeleka kwa fundi ili iondolewe GPRS, lakini fundi huyo alishindwa kuondoa kifaa hicho.
GPRS ni mfumo wa mawasiliano unaotumika pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa GPS kwa lengo la kutambua mahali kilipo chombo cha usafiri.
Hukumu hiyo imetolewa Jumatano Agosti 27, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya alipewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji.
Hakimu Lyamuya amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.
“Upande wa mashtaka umethibitisha shtaka la mauaji pasi na kuacha shaka baada ya kuleta mashahidi 13 ambao wametoa ushahidi wao Mahakama hapa,” amesema Hakimu Lyamuya.
Akichambua baadhi ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, Hakimu Lyamuya amesema mshtakiwa ndio aliyesababisha kifo cha Peya baada ya kumkodi na kwenda naye kwa wenzake wawili ambao ndio walitekeleza mauaji kwa kumpiga na kitu kizito kichwani na fuvu kupasuka.
Hakimu Lyamuya amesema, shahidi wa saba wa upande wa mashtaka F. 5818 Sajent Samwel ndio aliyemchukua maelezo ya onyo ya Othman.
Amesema katika maelezo yake Sajent Samuel alisema, Othman alimwambia alikuwa na wenzake wawili ambao ni Juma Shehe na Abilah ambao walikutana na kupanga mpango wa kwenda kupora pikipiki.
Hata hivyo, Shehe na Abilah hawajawahi kukamatwa wala kufikishwa mahakamani.
Amesema Othman ndio aliyekwenda kukodi pikipiki aina ya Boxer iliyokuwa inaendeshwa na dereva Peya na kumuelekeza kuwa anatakiwa ampeleke eneo la njia ya Ngo’mbe lililopo Temeke, ambapo alikuwa anakutana na Shehe na Abilah
” Baada ya kufika eneo walilopanga kukutana na mwenzake, mshtakiwa alimwambia dereva wa bodaboda simama na kisha kuchomoa funguo ya pikipiki,” amesema Hakimu, wakati akichambua ushahidi wa Sajent Samuel na kuongeza;
” Mshtakiwa baada ya kuchomoa funguo, wenzake walitokea eneo hilo ambapo Juma alimchoma kisu dereva wa bodaboda na kumpiga na kitu kizito kichwani na kudondoka chini,” amesema.
Amechambua kuwa, baada ya Peya kudondoka chini, Othman alichukua bodaboda hiyo na kuipeleka kwa fundi GPRS, huku akiwaacha wenzake wawili wakiendelea kumshughulikia Peya.
Katika maelezo yake, Othman alimueleza Sajent Samuel kuwa aliipeleka bodaboda hiyo kwa mtoa mdudu au mtoa GPRS ambaye ni fundi wa kutoa GPRS kwenye bodaboda, ambao wenyewe wanamuita mdudu.
Hata hivyo, fundi huyo alishindwa kutoa GPRS, na mshtakiwa aliondoka na kwenda nyumbani kwa mpenzi wake aitwaye Hadija, ambapo alipofika aliiegesha pikipiki hiyo nje ya nyumba na kisha kuingia ndani na kupumzika na mpenzi wake.
Amesema baada ya muda mfupi, kundi la bodaboda wakiwa na askari polisi walifika eneo hilo na kuichukua bodaboda hiyo.
Hata hivyo, baada ya siku kadhaa kupita, mshtakiwa huyo alikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa eneo la Sinza (Dar es Salaam) na kupelekwa kituo cha Polisi Chang’ombe (Dar es Salaam) kwa ajili ya mahojiano.
Na katika mahojiano yake Polisi, mshtakiwa alidai hajahusika na mauaji hayo, bali aliyehusika ni Juma Shehe.
Hakimu Lyamuya pia alichambua ushahidi wa daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) aliyeshiriki kuufanyia uchunguzi mwili wa Peya, ambaye alithibitisha kuwa amefariki dunia kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kusababisha fuvu lake kupasuka.
Akitoa adhabu, hakimu Lyamuya amesema; “Mshitakiwa ulishiriki kwenda kukodi bodaboda na kumpeleka kwenye mtego na kusababisha kifo chake, hakuna popote kuwa ulimshambulia marehemu, mchango wako ni kumpeleka katika mtego,” amesema Hakimu Lyamuya na kuongeza;
“Mshtakiwa mchango wako ni mkubwa katika kufanikisha mauaji ya Mahmud Peya, kwa kushirikiana na hao wenzako wawili ambao hawajapatikana mpaka sasa,” amesema Hakimu Lyamuya.
Akitoa hukumu, hakimu Lyamuya amesema ushahidi uliomtia hatiani mshtakiwa ni wa kimazingira, maelezo ya onyo na mashahidi wa upande wa mashtaka, vyote hivyo vimeoana na hivyo Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa.
“Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia, chini ya kifungu namba 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu na kifungu hiki adhabu yake ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa,” amesema Hakimu Lyamuya.
Awali, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na kusababisha mauaji ya mtu ambaye hana hatia na iwe fundisho kwa vijana.