Miaka 17 iliyopita, Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, nchini Kenya imekuwa zaidi ya kituo cha matibabu kwa Mtanzania, Selina Paul. Imekuwa ndiyo makazi pekee aliyoyajua kwa takribani miongo miwili.
Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Daily Nation, Selina alilazwa hospitalini hapo Machi, 2008 baada ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa wa schizophrenia (ugonjwa wa tatizo la afya ya akili unaoathiri namna mtu anavyofikiri, kuhisi na kutenda).
Wakati huo, Selina alikuwa na umri wa miaka 36 akiwa dhaifu, mwenye kuchanganyikiwa na akiwa mbali na nyumbani. Kulazwa kwake kwa muda mfupi kukageuka kuwa miaka katika wodi ya wagonjwa wenye tatizo la afya ya akili.
Hata baada ya hali yake kuimarika, hospitali haikuweza kumruhusu kuondoka. Bila jina kamili, anuani wala familia inayojulikana, Selina akawa mkazi wa hospitali pasipo kukusudia.
Hata hivyo, Jumanne (Agosti 26, 2025), akiwa na umri wa miaka 53, alitoka hospitalini si kama mgonjwa tena, bali amepona kabisa na yuko tayari kurejea nyumbani.
Familia yake, ambayo hospitali ilijaribu kuifikia kwa muda mrefu bila mafanikio, hatimaye ilipatikana jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Muunganiko wa familia ulikuwa wenye hisia. Kaka yake Phillipo Ombae aliyesafiri kutoka Tanzania Agosti 24, alisema walijulishwa na hospitali hiyo wiki mbili zilizopita, kwamba Selina alikuwa amelazwa hapo.
Ombae alishindwa kujizuia kutokwa machozi alipomkumbatia dada yake. Alisema familia yao ilimtafuta kwa muda wote huo na kuna wakati ilipoteza tumaini la kumpata.
Alikumbuka mara ya mwisho walipoonana na Selina ilikuwa mwaka 2005, kabla hajapotea baada ya kuanza kuugua kutokana na changamoto ya afya ya akili. Familia ilimtafuta pasipo kuchoka kwa kuzitembelea hospitali na mochwari mbalimbali.
“Wakati wote tulidhani amekufa. Tulipoteza tumaini la kumpata akiwa hai. Tunashukuru uongozi wa hospitali na kila mtu aliyemtunza dada yangu kwa miaka yote hii. Pia tunawashukuru wote mliojitoa kumrejesha kwetu. Yuko salama na mwenye furaha, nasi pia tuna furaha,” alisema Ombae na kuongeza:
“Selina alizaliwa katika Kijiji cha Maganjwa lakini baadaye aliolewa na kuishi Kijiji cha Sabilo wilayani Babati. Sherehe kubwa inamsubiri Tanzania, ambako watoto wake wanane na ndugu wengine wanamsubiri kwa hamu.”
Ombae pia aliishukuru hospitali kwa malezi waliyompa mtoto wa Selina, ambaye alikuwa na miezi sita tu wakati mama yake analazwa. Mtoto huyo alilelewa na kituo cha watoto na sasa yuko kidato cha nne.
“Baada ya kumaliza mitihani yake, tutamsaidia kupata nyaraka muhimu ili asafiri kurudi nyumbani na hatimaye akutane na familia yake,” alisema.
Hospitalini, Selina hakuweza kuficha furaha yake alipowaona ndugu zake. Akitabasamu kwa furaha, alirudia mara kwa mara maneno: “Nimefurahi sana kwenda nyumbani,” huku lafudhi yake ya Kitanzania ikiwa bado ingalipo.
Kwa mujibu wa Caroline Ojuang, ofisa ustawi wa jamii na msaikolojia katika hospitali hiyo, Selina alifikishwa hapo na wasamaria wema kutoka Kaunti ya Baringo walikomkuta akizurura mitaani akiwa na mtoto wake wa kiume mgongoni.
Baada ya uchunguzi, alilazwa. Hata hivyo, alikuwa akitoa maelezo yenye utata kuhusu utambulisho wake.
“Alijitambulisha kwa jina la Rosa kutoka Tanzania lakini alikuwa akitoa taarifa zinazopingana, jambo lililosababisha kushindikana kufuatilia familia yake. Hivyo akawa anajulikana Rosa TZ,” anasema Ojuang.
Kwa miaka mingi, madaktari, wauguzi na watumishi wa ustawi wa jamii walijaribu kuunganisha simulizi yake bila mafanikio. Hatua kubwa ilifikiwa mwaka huu alipotaja mara kwa mara kijiji chake cha nyumbani huko Mbulu, Tanzania pamoja na majina ya ndugu zake na kanisa alilowahi kusali.
Kwa taarifa hizo, hospitali ilimtafuta Askofu wa Jimbo la Mbulu, ambaye alithibitisha maelezo hayo kupitia kumbukumbu za kanisa. Hatua hiyo hatimaye ilifanikisha kupatikana kwa familia yake.
“Mwanzoni familia ilikuwa na wasiwasi kuamini taarifa hizo,” anasema Ojuang.
Anasema muunganiko huo wa familia ulimgusa kwa hisia kubwa pia mtoto wa Selina, ambaye ndiye pekee aliyekuwa akimtembelea hospitalini kwa miaka hiyo yote.
“Kila alipomkuta mama yake akiwa mgonjwa aliondoka kwa huzuni akitokwa machozi. Sasa, kwa kupatikana familia ya mama yake amepata utambulisho wa asili yake,” anasema.
Hospitali imethibitisha kuwa kamati yake ya msamaha itafuta bili zote za matibabu ya Selina kwa miaka yote aliyokuwa hapo.