Azam kunogesha Mbeya City Day Sokoine

Wakati Mbeya City ikiendelea na maandalizi ya tamasha lake la ‘Mbeya City Day’, timu hiyo imesema inatarajia kujipima nguvu dhidi ya Azam FC ili kunogesha tukio hilo linalotarajiwa kufanyika Septemba 9 mwaka huu.

Kabla ya tukio hilo, timu hiyo itaanza kushiriki shughuli za kijamii ikiwa ni kuchangia damu kwenye Hospitali ya Igawilo, kutembelea watoto kwenye Hospitali ya Wazazi Meta na kutembelea kituo cha watoto yatima kilichopo Iwambi jijini hapa.

Mbeya City inatarajia kushiriki Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana misimu miwili mfululizo, ambapo kwa sasa timu hiyo inaendelea na kambi yake huko Mwakaleli nje ya jiji la Mbeya.

Akizungumza leo Agosti 27, 2025, Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota amesema hadi sasa maandalizi ya Mbeya City Day yanaendelea vizuri na mashabiki watarajie burudani.

Amesema katika tukio hilo, wanatarajia kuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC, ambapo mbali na kuwapa raha mashabiki, wachezaji watapa ushindani kutoka kwa wapinzani.

“Tukizungumzia timu bora Tanzania, Azam huiachi, hivyo tunatarajia mchezo huo utakuwa kipimo bora kwa wachezaji lakini kutoa burudani kwa wadau na mashabiki wetu, lakini tutakuwa na uzinduzi wa jezi.

“Kabla ya Mbeya City Day, tutaanza na shughuli za kijamii, ambapo tarehe 3 tutaanza na utoaji damu pale Hospitali ya Igawilo, siku inayofuata tutakuwa Iwambi kituo cha watoto yatima kwani tunazo baraka zao,” amesema Mwankota.

Mwankota ameongeza kuwa, baada ya kurejea Ligi Kuu, uongozi umejitahidi kutengeneza kikosi bora na chenye ushindani ambapo msimu ujao wanahitaji nafasi saba za juu na kurejesha ubora wa timu hiyo.

Amesema baada ya misimu miwili mbele, timu hiyo itakuwa inapambania nafasi mbili za juu kwa ajili ya kusaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika akitamba kuwa mipango waliyonayo hawaoni kizuizi.

“Niwaombe mashabiki na wadau nje na ndani ya Mbeya timu yao imerejea kwa nguvu, waje kuisapoti na mkakati wetu ni kumaliza nafasi saba za juu kisha kusaka kimataifa huko mbeleni,” amesema Mwankota.