Baltasar Engonga ahukumia minane jela

Dar es Salaam. Mahakama nchini Guinea ya Ikweta imemhukumu aliyekuwa mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Fedha (NFIA), Baltasar Engonga kwenda jela miaka minane kwa ubadhirifu wa fedha za umma na kujitajirisha kinyume cha sheria.

Ikumbukwe Engonga aligonga vichwa vya habari duniani mwaka jana 2024 baada ya kusambaa kwa kasi kwa kanda za ngono  zilizohusisha wanawake tofauti tofauti wakidaiwa kuwa zaidi ya 400.

Video hizo za ngono zilizopatikana kwenye vifaa vyake vya kielektroniki vilivyokamatwa ikiwemo kompyuta mpakato wakati wa uchunguzi wa makosa ya matumizi mabaya ya fedha za umma baadhi ya waliokuwamo kwenye video hizo walikuwa wake wa maofisa wengine wa serikali.

 Kwa mujibu wa BBC na DW, Engonga alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi, vyombo vya habari vya ndani vya Equatorial Guinea vinaripoti.

” Mahakama ya mkoa wa Bioko jana Jumanne, Agosti 26, 2025 imempata Engonga na maofisa wakuu watano wa serikali na hatia ya kufuja maelfu ya pesa za umma kwa ajili ya taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta,” imenukuliwa.

Baada ya miezi kadhaa kuzuiliwa, mahakama ya mkoa wa Bioko ilimpata Engonga pamoja na wakurugenzi wakuu wengine wa wizara ya fedha na hatia ya utakatishaji fedha kwa ajili ya matumizi ya kibinafsi, pamoja na ubadhirifu wa gharama zenye thamani ya mamia ya maelfu ya dola.

Mahakama imewahukumu kifungo cha miaka minane jela na kuwaamuru walipe mamilioni ya faini kwa hazina ya umma.

Kwa uamuzi huo, mahakama imewatia hatiani waliokuwa wakurugenzi wakuu, Mangue Monsuy Afana, Baltasar Ebang Engonga Alú, na Rubén Félix Osá Nzang, kama wahusika wa uhalifu wa ubadhirifu wa fedha za umma.