Chuo cha FDC chaonyesha faida za miaka minne ya kutumia nishati safi

Rombo. Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mamtukuna (FDC) wilayani Rombo ni miongoni mwa taasisi zinazotekeleza mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kulinda afya na mazingira.

Chuo hicho chenye wanafunzi 460 kilianza kutumia gesi ya LPG mwaka 2021, baada ya kubaini madhara yaliyokuwa yakiwapata wahudumu wa jikoni kutokana na moshi wa kuni, yakiwemo muwasho wa macho, kikohozi na matatizo ya upumuaji.

Mkuu wa Chuo, Herry Kinyamagoha Mjengelaungu, amesema mabadiliko hayo yameleta matokeo chanya.

“Awali, wahudumu walikuwa wakiomba ruhusa mara kwa mara kwa ajili ya matibabu. Tangu tuanze kutumia gesi, changamoto hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa. Ingawa gharama ni kubwa zaidi ikilinganishwa na kuni, tumechagua kuendelea kwa sababu ya faida zake kiafya na kimazingira,” anasema.

Kwa maelezo yake, mtungi wa gesi unaogharimu Sh3.1 milioni hudumu kwa siku 45, ilhali lori la kuni la Sh300,000 lilitosha kwa miezi miwili. Hata hivyo, anasema chuo kimeamua kuwekeza kwenye gesi ili kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira salama.

Evaline Mushi, mhudumu wa jikoni, anasema gesi imepunguza matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanasababishwa na moshi wa kuni.

“Tangu tuanze kutumia gesi, afya zetu zimeimarika na chakula kinaiva kwa haraka,” anasema.

Naye Haikael Mduma, mhudumu mwingine, anasema gesi imeondoa kero za kuni ambazo mara nyingi zilikuwa mbichi na kuchelewesha upikaji.

“Kwa sasa tunapika chakula cha wanafunzi 450 hadi 500 ndani ya saa moja na nusu, tofauti na zamani ambapo tulihitaji zaidi ya saa sita. Pia tumepunguza kabisa changamoto za kiafya,” anasema.

Naye Amani Emmanuel, mwanafunzi wa chuo hicho, anasema matumizi ya nishati safi yameboresha maisha yao chuoni.

“Tunapata chakula kwa wakati na mazingira yamekuwa bora zaidi. Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya elimu na ustawi wetu,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, anasema wilaya hiyo imeweka mkakati wa kusambaza mitungi ya gesi kwa taasisi zenye watu zaidi ya 120 kama shule, magereza, na vyuo.

“Tumeshaondoa matumizi ya kuni katika baadhi ya magereza na taasisi za elimu. Pia tumeongeza juhudi za upandaji miti na kuhamasisha wananchi kutumia nishati mbadala,” anasema.

Anaeleza kuwa wilaya hiyo imeshirikiana na vyama vya akiba na mikopo (Amcos) kuuza majiko ya umeme kwa gharama nafuu, ambayo yanatumia umeme kidogo zaidi kuliko kutumia kuni au mkaa.

“Serikali imetoa ruzuku na kwenye baadhi ya maeneo, tumegawa bure majiko rafiki kwa mazingira, hususani kwa mama lishe,” anasema DC Mwangwala.

Kwa hatua hizi, Rombo imekuwa mfano wa utekelezaji wa sera ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikilenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.