Buhigwe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango, ameipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha huduma za kifedha nchini, hatua inayowezesha wananchi wengi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi.
Akizindua rasmi tawi jipya la benki hiyo leo Agosti 27,2025 wilayani Buhigwe, Dk Mpango amesema hatua ya benki hiyo kusambaza huduma katika halmashauri zote nchini ni msingi muhimu wa kuongeza ushirikishwaji wa kifedha kwa Watanzania.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kurasimisha shughuli za kiuchumi za wananchi wetu. Upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo wanayoishi wananchi ni kati ya nguzo kuu za kuwashawishi kurasimisha shughuli zao. Nawapongeza CRDB kwa kuhakikisha mnafika kila kona ya nchi kupitia matawi na mawakala wenu,” amesema Makamu wa Rais.
Amesisitiza kuwa changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi zinaweza kupungua iwapo wananchi wengi zaidi watajumuishwa kwenye mifumo rasmi ya kifedha. Hivyo, ushiriki wa sekta binafsi, hususan benki za biashara, ni muhimu sana katika mchakato huo.
Aidha, Dk Mpango ameipongeza CRDB kwa ubunifu wake katika huduma zinazozingatia imani na utamaduni wa Watanzania, akitoa mfano wa huduma ya CRDB Al Barakah Sukuk hatifungani inayofuata misingi ya sharia.
“Ninaamini wananchi wa Buhigwe, Kigoma na nchi nzima watatumia fursa hii kuwekeza na kuimarisha uchumi wao. Tawi hili litawapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki,” amesema.
Akiendelea, Makamu wa Rais aliwataka viongozi wa benki kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kuelewa kwa undani bidhaa na huduma zinazotolewa, hususan uwekezaji kupitia hatifungani. Alipendekeza pia kutumia wasanii maarufu kufikisha elimu hiyo kwa jamii kwa lugha rahisi na yenye ushawishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo huwatanguliza wateja mbele, ndiyo maana imekuwa ikipanua huduma zake kila mwaka. Alibainisha kuwa hadi Juni 2025, CRDB ilikuwa imepokea amana za zaidi ya Sh14 trilioni na kutoa mikopo ya Sh12.25 trilioni.
“Tulipoanza miaka 30 iliyopita tulikuwa na matawi 19 pekee, leo hii tumefikia zaidi ya matawi 260, yakiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hivi karibuni tutafungua Dubai. Huduma zetu zinawafikia wateja milioni sita nchini kote,” alisema Nsekela.
Amesema benki hiyo kupitia CRDB Bank Foundation imewafikia wananchi zaidi ya milioni moja kwa kutoa elimu ya fedha, ujasiriamali na mtaji kupitia programu ya Imbeju. “Lengo letu ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayepitwa na fursa hizi za kifedha,” amesisitiza.
Katika sekta ya kilimo, amesema benki hiyo imeshiriki kuwezesha ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kusaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo.
Akizungumzia wajibu wa benki kwa jamii, Nsekela amesema CRDB hutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kila mwaka kwa ajili ya miradi ya elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Katika hafla hiyo, CRDB ilikabidhi madarasa mawili, ofisi ya mwalimu mkuu, meza 80 na viti 80 kwa Shule ya Sekondari Kibande, na kuahidi kupeleka magodoro 150 kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita. Benki hiyo pia imewahi kutoa msaada wa madawati yenye thamani ya zaidi ya Sh17 milioni kwa shule mbalimbali mkoani Kigoma.
“Benki ya CRDB ndiyo kubwa zaidi nchini na ya tatu kwa ukubwa ukanda wa Afrika Mashariki. Lengo letu ni kuwa namba moja. Tutaendelea na ubunifu na kuwekeza kwenye jamii kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema Nsekela.