DKT MPANGO AIOMBA BENKI YA CRDB KUTOA ELIMU YA FEDHA AKIZINDUA TAWI BUHIGWE

Buhigwe. Tarehe 27 Agosti 2025: Akizindua tawi la Benki ya CRDB wilayani Buhigwe pamoja na kupokea madarasa mawili ya shule ya sekondari, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ameisifu Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kutanua huduma jambo linalosaidia kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi kwa wananchi.


Mheshimiwa Makamu wa Rais amesema kitendo cha kuwa na matawi katika halamashauri zote nchini kinaifanya Benki ya CRDB kuwafikia wananchi wengi zaidi kutoka katika kila pembe ya nchi. Kutokana na kuwapo kwa matawi ya benki pamoja na mawakala waliotapakaa maeneo mbalimbali, amesema kunasaidia kuwajumuisha wananchi wengi katika huduma za fedha.


“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kurasmisha shughuli za kiuchumi za wananchi wetu. Upatikanaji wa huduma za uhakika za fedha katika maeneo waliyopo wananchi ni kati ya nguzo muhimu zitakazowashawishi wananchi kurasmisha shughuli zao. Nawapongeza Benki ya CRDB kwa kuhakikisha mnakuwepo katika kila halmashauri nchini ili kufikisha huduma zenu kwa wananchi,” amesema Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais amesema changamoto nyingi zilizopo katika jamii zitaondoka iwapo wananchi wengi zaidi watajumuishwa kifedha na shughuli nyingi za kiuchumi zitarasmishwa hivyo ushiriki wa sekta binafsi hasa benki za biashara na taasisi za fedha ni muhimu sana katika kufanikisha hilo. Licha ya kuwa na matawi nchi nzima, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia ameipongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu wake kwenye huduma na bidhaa inazotoa kwa wateja wake zinazozingatia maadili, utamaduni mpaka imani zao za kidini.


“Mkurugenzi ameeleza hapa kwamba sasa hivi wanayo CRDB Al Barakah Sukuk ambayo ni hatifungani inayozingatia misingi ya sharia. Hii ni hatua kubwa ya kuwajali wawekezaji hasa kipindi hiki benki inaapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwenu. Naamini wana Buhigwe, Kigoma na Tanzania nzima wataitumia fursa hii kuwekeza ili kuimarisha uchumi wao. Tawi hili ninalolizingua leo naamini litaleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Buhigwe ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki,” ameeleza Mheshimiwa Dkt. Mpango.


Kati ya vitu alivyoviomba kwa benki za biashara zikiongozwa na Benki ya CRDB ni kutoa elimu ya fedha. Amesema wananchi wanapaswa kuelimishwa kwa kina kuhusu huduma na bidhaa za kisasa zinazotolewa na benki ili ziwanufaishe wananchi ambao ndio walengwa.

“Benki ya CRDB mmekuwa mnatoa hatifungani ikiwamo hii ya sasa hivi mnayoendelea kuiuza ya CRDB Al Barakah Sukuk lakini ni watu wachache sana wanaelewa maana ya hatifungani na namna wanavyoweza kunufaika nazo. Nawasihi mtoe elimu ya huduma zote mlizonazo pamoja na fursa za uwekezaji mnazozileta kwa wananchi,” amesema Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais amependekeza kutumiwa kwa wasanii ambao hueleweka kwa urahisi zaidi na wananchi kutoa elimu ya fedha, miongoni mwa mbinu zitakazosaidia kufanikisha mkakati wa kufikisha elimu kwa umma.


Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kila wakati benki huwatanguliza mbele wateja wake ndio maana imekuwa ikihakikisha inawafuata mahali popote walipo jambo linaloongeza imani yao.

“Mpaka Juni 2025, Benki yetu ilikuwa imepokea amana za wateja kiasi cha shilingi trilioni 14 na kukopesha jumla ya shilingi trilioni 12.25. Katika kipindi cha miaka 30 cha uwepo wa Benki yetu ya CRDB, tumekua na kutanua mtandao wetu wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka zaidi ya 260 tukilijumuisha hili tunalolizindua leo. 

Matawi haya yanatuwezesha kuhudumia zaidi ya wateja milioni sita nchini kote. Huduma zetu zimefika nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na hivi karibuni tutafika Dubai. Juhudi hizi zote zinadhihirisha jinsi tunavyowajali wateja wetu waliopo ndani na nje ya nchi na ndio maana halisi ya kaulimbiu yetu ya ‘ulipo tupo,’” amesema Nsekela.


Ili kuhakikisha wananchi wengi wanakuwa na uelewa mkubwa zaidi, Nsekela amesema Benki ya CRDB ilianzisha kampuni tanzu ya CRDB Bank Foundation ambayo inatoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwapa mtaji wezeshi wale wanaokidhi vigezo kupitia Programu yake ya Imbeju.


Kupitia programu hii, amesema CRDB Bank Foundation imewafikia zaidi ya wananchi milioni moja na juhudi za kuwafikia wengi wengine zinaendelea ili kuhakikisha hakuna anayeachwa wala kupitwa na fursa hizi za kukuza kipato binafsi na kushiriki kuujenga uchumi wa taifa.

“Benki ya CRDB ndio kubwa zaidi nchini na ya tatu kwa ukubwa ukanda wa Afrika Mashariki, lengo letu ni kuwa namba moja hivyo tutaendeleza ubunifu kwa manufaa ya wateja wetu na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema Nsekela.


Licha ya kushiriki kutimiza malengo ya mtu mmojammoja, Nsekela amesema Benki ya CRDB inashiriki pia kutatua changamoto za kitaifa akitolea mfano ujenzi wa kiwanda cha mbolea jijini Dodoma.  


“Mbolea ni kati ya changamoto tulizonazo kwenye sekta ya kilimo. Najivunia kusema kwamba Benki ya CRDB imeshiriki kuwezesha ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Burundi. Hili pekee linaonyesha namna tunavyokuza diplomasia ya uchumi. Kwa sasa tunayo CRDB Al Barakah Sukuk, hatifungani inayofuata misingi ya sharia inayompa kila fursa kila Mtanzania kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani kwa faida ya asilimia 12 kwa mwaka,” amesema Nsekela.

Akizungumzia kuhusu uwekezaji kwa jamii, Nsekela amesema Benki ya CRDB hutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kila mwaka ili kuwekeza kwenye miradi ya wananchi hasa iliyopo kwenye sekta ya elimu, mazingira, afya na uwezeshaji wa wanawake na vijana. 

“Leo tunakabidhi madarasa mawili, ofisi ya mkuu wa shule, viti 80 na meza 80. Hata hivyo, tumegundua kuna changamoto ya malazi shuleni hapa hasa kwa wanafunzi waliopo kwenye madarasa ya mitihani. Benki yetu ya CRDB italeta hapa magodoro 150 kwa ajili ya wanafunzi hawa wanaosoma katika Sekondari hii ya Kibande,” amesema Nsekela.

Licha ya msaada huo uliotolewa kwa Shule ya Sekondari kibande, Benki ya CRDB ilishapeleka madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.35 kwa Shule Msingi Kasebuzi iliyopo wilayani Kibondo, madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 3.75 kwa Shule Msingi Ruyenzi ya Kakonko, madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.4 kwa Shule ya Nguruka ya Uvinza, na  madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.075 kwa Shule Msingi Sokoine ya Kigoma Vijijini pamoja na madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 4 Shule Msingi Kabulazili ya Kasulu Mjini.