Kilombero. Jumla ya kaya 1,800 kutoka vijiji viwili vya Kata ya Mofu, wilayani Kilombero, zinatarajiwa kunufaika kiuchumi na kijamii baada ya kupatiwa miche ya bure ya matunda na kokoa kupitia Mradi wa Mazingira Plus, unaoratibiwa na Taasisi ya Mofu Rothenburg.
Hatua hiyo inalenga kusaidia juhudi za kuhifadhi mazingira sambamba na kuinua kipato cha wananchi wa maeneo husika.
Mratibu wa mradi huo, Michael Mairinga, ametaja vijiji vinavyohusika kuwa ni Ikwambi na Mofu, na kufafanua kuwa pamoja na kaya kunufaika moja kwa moja na ugawaji wa miche hiyo, taasisi za kijamii zikiwemo zile za kidini na za kiserikali zilizopo katika vijiji hivyo pia zitapata mgao wa miche hiyo ili kuhakikisha ushirikishwaji wa jamii nzima katika utekelezaji wa mradi.
Kwa mujibu wa Mairinga, mradi huo pia unalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa mazingira, kilimo endelevu na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kupitia matumizi bora ya rasilimali zilizopo.
“Taasisi imenunua miche 19,000 ya matunda na miche 30,000 ya kokoa kwa ajili ya kugawa bure kwa wananchi na taasisi hizi na mradi huu utakuwa wa miaka miwili,” amesema Mairinga.
Amebainisha kuwa taasisi za Serikali zitakazofainika na miche hiyo ya miti ni shule sita za msingi na shule mbili za sekondari pamoja na makanisa, misikiti na zahanati.
Mairinga amesema lengo la mradi huo ni kurudisha uasili wa mazingira ya Mofu ambayo zamani ilikuwa ya kijani huku akitaja vipaumbele vya mradi huo kuwa ni ikolojia ya kilimo, usimamizi wa rasilimali za asili, kuongeza kipato kwa wananchi na usafi wa mazingira.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mofu Rothenburg, Reinfred Magungu amesema matarajio yao baada ya mradi huo kukamilika ni kuona hali ya mazingira katika maeneo hayo ikiimarika.
Magungu amesema pamoja na kuanzisha mradi huo mpya pia taasisi hiyo inafanya shughuli nyingine katika kata hiyo ikiwemo kusaidia vijana wanaoishi katika mazingira magumu, kwa kuwapatia ada na vifaa vya shule kuanzia kidato cha kwanza hadi chuo kikuu.
Miradi mingine ni wa kilimo ambao unasaidia vikundi vinane vya wakulima wa zao la mpunga kwa kuwajengea ghala, na mradi wa chuo cha ufundi ambacho kinatoa fani nne za ufundi bure zikiwemo uashi, ushonaji, umeme na uchomeleaji na kuongezewa fani ya kilimo.