Mhadhiri aliyeshtakiwa kwa madai ya rushwa ya ngono kizimbani tena

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Tabora, imebatilisha uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Tabora iliyomuachia huru, Michael Mgongo, aliyeshtakiwa kwa kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake kwa lengo la kumpendelea katika mitihani.

Mahakama imebatilisha uamuzi uliofikiwa na mahakama ya chini ambayo ilimuachia huru Mgongo, mhadhiri msaidizi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) baada ya kumuona hana kesi ya kujibu.

Mahakama Kuu imeamuru shauri hilo kurejeshwa mahakamani mbele ya hakimu yuleyule ili kuendelea na kesi pale alipoishia kabla ya kutoa uamuzi kuwa mshtakiwa hana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo umetolewa Agosti 22, 2025 na Jaji Zainabu Mango aliyesikiliza rufaa iliyokatwa na Jamhuri.

Mahakama ya Wilaya Tabora iliamua kwamba, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa, hivyo ilimwachia huru kwa sababu hakuwa na kesi ya kujibu.

Mgongo alishtakiwa akidaiwa kati ya Desemba 2022 na Mei 10, 2023 ndani ya Manispaa ya Tabora, akiwa Mhadhiri Msaidizi katika Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), tawi la Tabora aliomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake (jina linahifadhiwa), ili kumpendelea kwenye mitihani ya chuo.

Mshtakiwa alikana shtaka. Wakati wa usikilizwaji, upande wa mashtaka uliita mashahidi wanne lakini mwathirika hakufika mahakamani kutoa ushahidi.

Jitihada za kumwita mwathirika kutoa ushahidi ziligonga mwamba, shauri likaahirishwa mara tatu mfululizo.

Hatimaye, Mahakama iliandika uamuzi na kusema: “Kwa kuzingatia sababu nilizotoa, nimeridhika kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa. Hivyo, mshtakiwa hana kesi ya kujibu na kwa hiyo hana hatia ya shtaka la kuomba rushwa ya ngono.”

Kwa kutoridhika na uamuzi huo, Jamhuri ilikata rufaa ikiwa na sababu mbili; Kwanza, hakimu alikosea kisheria na kiukweli kwa kufunga kesi ya upande wa mashtaka kabla ya mwathirika (shahidi muhimu) kutoa ushahidi mahakamani.

Pili, hakimu alikosea kisheria na kiukweli kwa kumwachia huru mshtakiwa baada ya kuamua kuwa hana kesi ya kujibu ilhali hakimu mwenyewe ndiye alifunga kesi ya upande wa mashtaka kabla ya mwathiriwa kutoa ushahidi wake.

Wakati shauri lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Salyungu Kibinza, huku mshtakiwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Akram Magoti.

Katika kuunga mkono rufaa, Kibinza alijumuisha hoja zote mbili na kueleza kuwa, wakati wa usikilizaji upande wa mashtaka uliwaita mashahidi wanne.

Hata hivyo, kumbukumbu za mahakama zinaonyesha hakuna mahali ambako upande wa mashtaka ulifunga kesi yake. Ni Mahakama yenyewe iliyofunga kesi ya mashtaka na kutoa uamuzi. Aliiomba mahakama itengue amri ya kumwachia huru mshtakiwa na kuamuru shauri liendelee pale lilipoishia, mbele ya hakimu mwingine.

Wakili Magoti alipinga rufaa hiyo akidai Jamhuri ilishindwa kumleta shahidi mara tatu mfululizo, hivyo uamuzi wa mahakama ulikuwa sahihi.

Alieleza mahakama ilitumia mamlaka yake kudhibiti mwenendo wa shauri, akisisitiza kuwa haki ya usikilizwaji wa haki, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya nchi, inahusu pande zote mbili.

Hata hivyo, wakili Magoti alikubali kwamba mahakama ilipaswa kuamua kama kuna kesi ya kujibu au la, pale upande wa mashtaka unapokuwa umefunga kesi yake. Alikiri kuwa mahakama ilijielekeza yenyewe kimakosa, badala yake ilipaswa kufuta mashtaka dhidi ya mshtakiwa.

Aliomba shauri lirejeshwe kwa hakimu yuleyule ili liendelee pale lilipoishia.

Baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, jaji amesema hakuna ubishi kwamba mahakama ya awali haikupaswa kutoa uamuzi wa hakuna kesi ya kujibu wakati ambao upande wa mashtaka haujafunga kesi yake.

“Kumbukumbu zinaonyesha hakimu aliandika uamuzi kabla ya upande wa mashtaka kufunga kesi yake. Swali muhimu je, hakimu alikuwa sahihi kufanya hivyo?” amesema.

Jaji amesema kumbukumbu zinaonyesha mashahidi wanne walishasikilizwa na vielelezo kuwasilishwa. Shahidi aliyefuata alikuwa mwathirika, ambaye hakuweza kufikishwa kwa mara tatu mfululizo (Novemba 4, 2024, Novemba 21 na Desemba 5), kwa sababu upande wa mashtaka haukuwa na shahidi.

“Baada ya hapo, mahakama ikaahirisha kwa ajili ya uamuzi bila sababu ya moja kwa moja. Ingawa kumbukumbu hazionyeshi, mahakama ilidhani kuwa upande wa mashtaka umefunga kesi, kisha ikaamua mshtakiwa hana kesi ya kujibu,” amesema jaji.

Akirejea uamuzi uliotolewa katika shauri la Abdallah Kondo dhidi ya Jamhuri, amesema Mahakama ya Rufaa ilishasema wazi kuwa, hakimu hana mamlaka kisheria kufunga kesi ya upande wa mashtaka au utetezi; pande zote mbili zina uhuru kufunga kesi zao zenyewe.

Katika shauri hilo ambalo liliahirishwa mara tatu, amesema mahakama haikupaswa kufunga ushahidi, hivyo kasoro hiyo ya kiutaratibu inatosha kuthibitisha kuwa rufaa ina mashiko.

“Kwa mazingira haya, ninaifuta na kutengua hukumu ya mahakama ya awali. Shauri linarejeshwa mahakama ya awali ili likaendelezwe na hakimu yuleyule kuanzia pale lilipoishia kabla ya kuandikwa kwa uamuzi wa hakuna kesi ya kujibu,” ameamuru na kuongeza:

“Kwa masilahi ya haraka ya haki na bila kuathiri haki za mshtakiwa, upande wa mashtaka unaamriwa kukamilisha na kufunga kesi yake ndani ya muda muafaka utakaopangwa na hakimu husika.”