Morocco, Madagascar patachimbika CHAN 2024

TIMU ya taifa la Morocco imeweka historia nyingine kwenye michuano ya (CHAN) 2024 baada ya kuibwaga Senegal kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya bao 1-1 katika dakika 120 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Kampala huku wakiwa na hesabu za fainali.

Hii ni mara ya tatu kwa Morocco kutinga fainali ya michuano hiyo, katika awamu mbili zilizopita walitwaa taji hilo moja wakiwa wenyeji, 2018 kwa kuifunga Nigeria mabao 4-0 na miaka miwili baadae walilitetea taji lao huko Cameroon kwa kuichapa Mali mabao 2-0.

Kocha wa Morocco, Tarik Sektioui, alieleza furaha na faraja kwa kikosi chake baada ya mchezo huo mgumu.

“Tulijua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu tulikabiliana na mabingwa watetezi. Hawa vijana wa Senegal wana nguvu, kasi na nidhamu. Lakini nilisema kabla ya mechi, uzoefu wetu na utulivu katika nyakati ngumu unaweza kutupa faida, na hilo ndilo lililotokea. Penalti ni sehemu ya mchezo, na wachezaji wangu walionesha utulivu mkubwa,” alisema.

Sektioui aliongeza kuwa maandalizi ya timu yake yamekuwa yakijikita zaidi kwenye uimara wa kimbinu kuanzia kichwani na katika nidhamu ya mchezo: “Tumekuwa tukifanya kazi siyo tu kwenye uwanja bali pia kwenye akili. Timu hii inajua presha za mashindano makubwa. Nilichowaambia kabla ya penalti ni kitu kimoja kuwa na utulivu na kuamini maandalizi yetu. Naona fahari kubwa jinsi walivyotekeleza.”

Kwa upande wake, kocha wa Senegal Souleymane Diallo hakuweza kuficha hisia baada ya timu yake kuondolewa kwenye mashindano, lakini alisifu utendaji wa vijana wake.

“Nimewaambia mara nyingi, hii ni timu changa sana. Walicheza kwa moyo na nidhamu hadi dakika ya mwisho. Tumepoteza kwa penalti, na penalti mara zote ni mchezo wa bahati nasibu. Kwa kiwango walichokionesha, naona fahari kubwa kwao. Wanastahili pongezi,” alisema.

Diallo alifafanua kuwa malengo ya Senegal hayajaishia hapa, na mechi ya kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Sudan itatumika kama sehemu ya kuendelea kukijenga kikosi hicho.

“Sasa tunafikiria mchezo dhidi ya Sudan. Tunataka kumaliza mashindano kwa heshima. Lakini zaidi ya yote, tunajua tumeanza safari ya kizazi kipya cha wachezaji. Leo siyo mwisho, ni mwanzo wa kitu kikubwa,” alisema

Sektioui aliendelea kueleza umuhimu wa ushindi huu kwa Morocco, akiweka wazi dhamira yao ya kurejesha taji la CHAN.

“Kila mmoja kwenye timu anajua thamani ya kombe hili. Morocco imekuwa na historia nzuri kwenye CHAN, na tunataka kuendeleza hilo. Tumefika fainali, lakini hatujamaliza kazi. Tunajua Madagascar siyo timu ya kubeza, wamethibitisha ubora wao kwa kuondoa timu ngumu. Itakuwa fainali yenye changamoto kubwa,” alisema.