Mukwala, Aucho watemwa The Cranes

WACHEZAJI Steven Mukwala na Khalid Aucho wameachwa katika kikosi cha nyota 28 wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2026, dhidi ya Msumbiji Septemba 5 na Somalia Septemba 8, 2025.

Mukwala anayeichezea Simba ametemwa sambamba na Aucho aliyemaliza mkataba wake na Yanga kisha kujiunga na Singida Black Stars, ambapo katika kikosi hicho cha The Cranes hakuna mchezaji yeyote aliyechaguliwa anayetokea kwenye Ligi Kuu Bara.

Hatua ya kutangazwa kwa kikosi hicho kipya, inajiri ikiwa ni siku chache tangu miamba hiyo ya soka kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kutolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya ndani (CHAN).

Uganda ambao ni wenyeji wa CHAN 2024, ikishirikiana na Tanzania na Kenya zilizotolewa zote, ilitolewa kufuatia kuchapwa bao 1-0 na bingwa mtetezi Senegal, iliyotolewa pia nusu fainali na Morocco kwa penalti 5-3, baada ya sare ya 1-1, dakika 120.

Katika kikosi cha wachezaji 28 wa The Cranes kilichoitwa ni makipa, Denis Onyango (Mamelodi Sundowns FC), Omar Jamal Salim Magoola (Richards Bay), Nafian Alionz (Defence Force SC) na Joel Mutakubwa anayeichezea BUL Jinja FC ya Uganda.

Mabeki ni Elvis Bwomono (IBV Vestmannaeyjar), Herbert Bockhorn (FC Magdeburg), Elio Capradossi (FC Universitatea Cluj), Rodgers Torach, Hilary Mukundane (Vipers FC), Toby Sibbick (Burton Albion FC) na Jordan Obita anayeichezea Hibernian.

Wengine ni Aziz Kayondo (FC Slovan Liberec), Herbert Achai na Gavin Kizito wanaoichezea KCCA FC, huku viungo ni Ronald Ssekiganda (APR FC), Kenneth Semakula (Al-Arabi), Joel Sserunjogi (KCCA FC) na Karim Watambala anayecheza Vipers SC.

Nyota wengine ni kiungo, Jamal Mutyaba anayechezea CS Sfaxien ya Tunisia, huku washambuliaji ni Omedi Denis wa APR FC, Allan Okello (Vipers SC), Mpande Joseph (PVF-CAND FC), Rogers Mato (FK Vardar), Reagan Mpande na Patrick Jonah Kakande wa SC Villa.

Washambuliaji wengine wanaoundwa kikosi hicho ni Jude Ssemugabi (Kitara FC), John Paul Dembe (BK Hacken) na Uche Ikpeazu anayeichezea St Johnstone FC ya Scotland na kuunda timu ya nyota 28 kwa ajili ya kuipambania kufuzu Kombe la Dunia 2026.