Mwabukusi: Hoja ya Chadema kuhusu ‘reforms’ ya kweli huwezi kuipuuza

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema yapo maeneo muhimu katika shughuli ya kuelekea uchaguzi mkuu yaliyotakiwa kufanyiwa marekebisho kutokana na changamoto zinazolalamikiwa, lakini hayakuguswa kufanyiwa marekebisho. 

Msingi wa kuyasema hayo unatokana na majadiliano na mijadala yaliyofanywa kati ya TLS na wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia juu ya kuelekea ushiriki wa usawa katika uchaguzi mkuu ujao. 

Kauli hiyo ameitoa jana Jumanne, Agosti 26, 2025 alipokuwa akieleza juhudi  zilizochukuliwa na TLS kuhakikisha kunakuwa na maridhiano na mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesema katika mkutano mkuu wa amani na maazimio wa Agosti 9, 2025 walikutana wadau wanaohusiana na masuala ya demokrasia na uchaguzi wakajadili kwa kina na wakaona kwa dhati kuna tatizo. 

“Si vyema kupuuza malalamiko yanayotolewa na watu tukaona ni muhimu kuundwa kwa kamati shirikishi ya uwakilishi mpana wa makundi yote ya kijamii kuainisha hatua za dharura za muda mfupi, wa kati na mrefu kwa ajili ya kuhakikisha haki amani na utawala bora unadumishwa nchini, pia changamoto zote za zoezi la uchaguzi zinapatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.”

“Kwa hiyo kilichozungumzika ni kwamba tatizo lipo na marekebisho yalifanyika lakini kuna maeneo muhimu ambayo yalitakiwa kufanyiwa marekebisho na yalikuwa na changamoto za kweli hayakuguswa,  kwa hiyo hoja ya Chadema kwamba kuna changamoto katika mabadiliko (reforms) ni halali huwezi kuipuuza,” amesema.