Mwili waopolewa mtaroni Jangwani | Mwananchi

Dar es Salaam. Mwili wa mtu mmoja umeonekana asubuhi ukielea majini kwenye mtaro uliopo Jangwani, jirani na kilipokuwa kituo cha mabasi ya mwendokasi.

Katika eneo hilo kwa sasa unaendelea ujenzi wa barabara mbadala kabla ya kubomolewa ya awali kupisha ujenzi wa daraja la juu litakalounganishwa eneo la Fire na Magomeni.

Mwili huo wa mtu mzima umeonekana leo Jumatano Agosti 27, 2025, hivyo kuzua taharuki kwa wananchi waliotumia Barabara ya Morogoro lililoko eneo la Jangwani.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (SACF), Peter Mabusi amesema walipata taarifa ya kuwepo kwa mwili huo saa 3:30 asubuhi, hivyo walituma timu kufuatilia.

Amesema timu hiyo ilikuta mwili wa mtu mzima aliyetambuliwa kwa jina la Swalehe Shukurani, ukiwa chini ya daraja lenye maji.

Amesema mwili huo uliopolewa na umekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Tulifanikiwa kuutoa mwili huo saa nne kasoro asubuhi na kukabidhi kwa wenzetu wa Jeshi la Polisi, umepelekwa Hospitali ya Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema.

Mabusi amesema mwili huo umetambuliwa na majirani zake waliofika eneo la tukio baada ya kusikia kuna mtu ameonekana chini ya daraja hilo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo amesema: “Kila tukio linalotokea jeshi linafanyia uchunguzi, hivyo tutatolea taarifa kamili uchunguzi ukikamilika.”

Kwa mujibu wa watu waliokuwapo eneo hilo, shuhuda wa kwanza alipofika usawa wa mtaro aliona kitu kinaelea kama vile mwili wa binadamu ndipo aliposogea, huku akiwaita wapitanjia wengine.

“Sikubahatika kuuona mwili, lakini wanasema mtu aliyeuona alikuwa mpitanjia. Aliona kitu kikielea mtaroni, aliposogea karibu alibaini ni mwili wa binadamu,” amesema Jumanne Seif akiwa eneo la tukio saa nne asubuhi.

Shuhuda mwingine, Irene Raphael, akizungumza na Mwananchi amesema wakiwa kwenye bajaji walimsikia mtu akisema kuna mwili upo mtaroni.

“Nilikuwa kwenye bajaji, tukaona watu wamejaa eneo la Jangwani, mara tukamsikia mtu akisema tayari wameshamaliza kazi ya Mungu. Ikabidi tuulize nini kimetokea, tukaambiwa kuna mtu ameuawa na kutupwa kwenye mtaro,” amesema.

Amesema hadi anaondoka eneo la tukio saa 3:22 asubuhi, hakuwa amewaona polisi, huku idadi ya watu ikiongezeka kwenda kushuhudia kilichotokea.

Mbali ya tukio hilo, Kamanda Muliro pia amesema tukio la mtoto kutoweka linafanyiwa uchunguzi na taarifa kamili itatolewa ukikamilika.

Katika tukio hilo inadaiwa watu waliokuwa kwenye pikipiki walimchukua mtoto Patrick Luzwilo, mwenye miaka miwili na nusu, mwanafunzi wa Shule ya Awali ya Vein Academy, iliyoko Goba.

Inaelezwa mtoto huyo alichukuliwa nyumbani kwao jana Agosti 26, 2025 saa 1:30 asubuhi, katika Mtaa wa Wakutiri, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Pascal Luzwilo, baba wa mtoto huyo alilieleza Mwananchi jana (Agosti 26) kuwa familia iliamka kama kawaida na kuanza maandalizi ya kumpeleka shuleni.

“Kila siku tunaamka wote pamoja, mama anamwandaa mtoto, kisha anajiunga na dada yake wanaposubiri gari la shule getini. Ni maisha ya kawaida, hatuna ugomvi na mtu wala mzozo wa biashara,” amesema.

Luzwilo amesema muda mfupi baada ya mtoto kutoka na dada yake walisikia kelele za majirani waliogonga geti wakisema mtoto wao amechukuliwa na pikipiki.

“Kwa kawaida mama humpeleka hadi getini, wakati mwingine mimi au dada yake. Lakini leo baada ya muda tukasikia kelele mlangoni, tukakimbia kuangalia, tukaambiwa mtoto amechukuliwa na watu wakiwa kwenye pikipiki na kukimbia,” amesema.