……………….
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetoa mafunzo kwa Maafisa wa Uthibiti Ubora, Wakuu wa Vyuo na Wakuu wa Idara kutoka vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika Kanda ya Mashariki, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa vyuo hivyo na kuhakikisha ubora wa mafunzo unaboreshwa ili kuzalisha wahitimu wenye sifa zinazohitajika katika soko la ajira.
Akizungumza leo, Agosti 27, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora kutoka NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo vinavyosimamiwa na NACTVET, hususan katika maeneo ya utoaji wa elimu na uandaaji wa mitaala.
Dkt. Oleke amesema kuwa Baraza litaendelea kusimamia ubora wa elimu katika vyuo vyote vilivyo chini ya NACTVET ili kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanafikia viwango vinavyotarajiwa.
“Kwa sasa tumeongeza viwango vya ubora kutokana na mahitaji ya soko la ajira. Hivyo, ni lazima wanafunzi wanaohitimu kutoka katika vyuo vya ufundi wawe wameandaliwa ipasavyo. Tumetengeneza miongozo inayoonesha viwango vya ubora vinavyotakiwa,” amesema Dkt. Oleke.
Kwa upande wake, Meneja wa NACTVET Kanda ya Mashariki, Dkt. Hirst Ndisa, amesema kuwa mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Uthibiti Ubora kutoka vyuo takribani 134 kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Dkt. Ndisa ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kupata elimu juu ya uthibiti ubora katika taasisi zao, ili wanapotoa mafunzo kwa wanafunzi, waweze kuwajengea ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri katika soko la ajira.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Ubora kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii, Bi. Elina Makanja, wameishukuru NACTVET kwa kutoa mafunzo hayo, wakisema kuwa yanawakumbusha umuhimu wa kudhibiti ubora katika taasisi zao, na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia.
“Natarajia katika mafunzo haya nitapata fursa ya kuelewa zaidi na kushirikiana na washiriki wengine katika kubuni mbinu mbalimbali zitakazosaidia taasisi zetu kutoa mafunzo yenye viwango vinavyotakiwa,” amesema Bi. Makanja.