Dar es Salaam. “Kamwe asiwepo mmoja wetu akawa chanzo cha kukiuka sheria, kanuni na taratibu wakati wote wa kampeni na baada ya kampeni ili kuepuka vurugu au uhalifu wa aina yeyote ile kutokea.”
Hiyo ni kauli ya Jeshi la Polisi Tanzania iliyotolewa kupitia msemaji wake, David Misime leo Jumatano Agosti 27, 2028 ikiwa zimesalia saa chache kabla ya kuanza kwa kampeni za wagombea wa urais, ubunge na udiwani kesho Agosti 28, 2025.
Kauli hiyo inakuja huku joto la uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 likizidi kupanda ikiwemo kuanza kwa kampeni hizo, ambapo tayari vyama vinavyoshiriki uchaguzi vikitangaza kuanza mikutano ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoanza kesho Kawe Dar es Salaam.
Kupitia taarifa hiyo Polisi imewajulisha wananchi na wadau wote kuwa, ipo tayari na imejiandaa vizuri ipasavyo kuhakikisha wanaendelea kuimarisha usalama wakati wote wa kampeni na baada ya kampeni.
“Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wagombea na wafuasi wao na wananchi wote kwa ujumla, kukumbuka jukumu la kudumisha amani, utulivu na usalama ni letu sote kama Watanzania.”
“Tunatoa wito kila mmoja azingatie ratiba na muda wa kampeni aliopangiwa ili kuepuka mivutano, migongano, migogoro au uhalifu kutokea kwani hatutasita kumchukulia hatua kama sheria za nchi zinavyoelekeza,” imeeleza taarifa ya jeshi hilo.
Tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), inaendelea kuwateua wagombea mbalimbali wa nafasi hizo wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi, kugombea nafasi ya urais na Makamu wa Rais Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza leo Jumatano jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, amesema wagombea waliopendekezwa na CCM wametimiza masharti yote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuthibitishwa rasmi kuwania nafasi hizo.
Uteuzi huo unawafanya Samia na Nchimbi kuingia rasmi katika kinyang’anyiro cha urais kuelekea uchaguzi mkuu.
Hata hivyo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa wagombea wawili wa urais wa Tanzania, Luhaga Mpina wa ACT-Wazalendo na Wilson Elias wa ADC, kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama vyao.
Uamuzi huo umetolewa usiku wa jana Jumanne, Agosti 26, 2025 wakati leo Jumatano ni siku ya mwisho ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi kwa nafasi za Rais, Makamu wa Rais, wabunge na madiwani, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni hizo kesho, kwa mujibu wa ratiba INEC.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Agosti 26, 2025 usiku na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu ya Uraia, Abuu Kimario, imeelezwa wagombea hao wamekiuka masharti ya Kifungu cha 4(5)(a) na (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 baada ya kubainika kuwa uteuzi wao haukufuata misingi ya sheria, katiba na kanuni za vyama vyao.