Dodoma. Mgombea wa kiti cha urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameshaingia Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kurudisha fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Rais Samia ameingia saa 1.50 asubuhi leo Jumatano Agosti 27, 2025 akiwa kwenye msafara wa magari machache tofauti na alivyoingia siku ya kuchukua fomu Agosti 9, 2025 na hakukuwa na shamrashamra nyingi.
Leo inakuwa mara ya pili kwa Rais Samia kufungua njia kwa wagombea wenzake ambapo wakati wa kuchukua fomu alikuwa wa kwanza pia kati ya vyama 18.
Baada ya kuingia, alishuka kwenye gari la kijani akiwa amevalia mavazi ya kijani ambayo ni maarufu kama sare ya chama chake na alipokewa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima.
Kabla ya msafara wake kaingia, ulitangulia msafara wa magari matatu moja likiwa na rangi ya kijani ambalo lilimbeba Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro.
Saa 2:36 asubuhi, Rais Samia alitoka ndani na ametumia dakika tatu akiwa amesimama na kuzungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Migiro, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi na katika msafara huo alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na viongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma walioongozwa na Mwenyekiti Alhaj Adam Kimbisa.
Ratiba iliyotolewa mapema leo na INEC inaonyesha vyama vyote 18 ambavyo wagombea wake walichukua fomu, vitarudisha kwa ajili ya kuomba uteuzi na kwenye ratiba hiyo mgombea wa ACT-Wazalendo Luhaga Mpina atafunga pazia.
Kuanzia kesho Alhamisi, Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 ni kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Endelea kufuatilia Mwananchi