::::::;;
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeendelea kutekeleza miradi ya nishati kwa kuunganisha wateja umeme katika maeneo ya vijijini ili kuboresha na kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi mkoani Manyara.
Hayo yamebaibishwa leo Agosti 27, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, sambamba na kuzungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA ambapo ameweza kushuhudia wananchi wakiunganishiwa huduma ya umeme kijiji cha Chemchem, Kitongoji cha Soraa mkoani Manyara.
“Sisi REA tayari tumekamilisha kupeleka umeme kwenye vijiji vyote 440 vya mkoa huu wa Manyara, sasa tunaendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote mkoani hapa ili wananchi wapate nishati ya umeme, ” Amesema Mhe. Balozi Kingu.
Wakati huohuo amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme mkoani humo kuhakikisha wanakamilisha miradi yao kwa wakati ili iweze kuleta tija kwa wananchi. Amesema kukamilika miradi kwa wakati ni fursa kwa wakandarasi kuweza kupata fursa nyingine ya kuaminiwa zaidi na Serikali hatimaye kupata miradi zaidi.
Halikadhalika amesisitiza kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuunganisha umeme katika vitongoji vyao pindi miradi hiyo inapokamilila ili umeme huo uweze kuwa na tija kwao na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi wa China Railway Seventh Group Company Limited (CRSG), Mha. Estheria Fumbuka, ametakiwa kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa wakati ikiwemo kufikisha nguzo kwa walengwa kufikia mwezi Septemba mwaka huu ili wananchi waunganishiwe umeme.
Naye, Mhandisi wa mradi kutoka Nakuroi Investment Company Limited, Mha. James James ametakiwa kuzingatia makubaliano yake ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo mkoani humo na REA ili miradi hiyo ikamilike katika muda uliopangwa ili kuwapunguzia adha wananchi kwa kukosa umeme katika maeneno yao na hatimaye wanufaike na nishati hiyo.
Miradi inayoendelea hadi sasa kutekelezwa mkoani Manyara ni pamoja na mradi wa ujazilizi awamu ya 2C (REDP 2C) kwa gharama ya shilingi bilioni 37.7 na mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji (HEP -2A) wenye thamani ya shilingi bilioni 13.7 kwa ujenzi wa miundombinu inayolenga kuongeza idadi ya kuunganisha umeme katika vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma mkoani Manyara.
*Mwisho*