KOCHA wa Madagascar, Romuald Rakotondrabe anapozungumza kuhusu timu yake, mara chache hugusia mchezaji mmoja mmoja na badala yake huweka msisitizo katika nidhamu, mshikamano na mtazamo chanya misingi ambayo imewapa nafasi ya kufika fainali ya CHAN.
Madagascar ambayo ilishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kund B nyuma ya Taifa Stars ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa bao 1-0 Sudan juzi, Jumanne kwenye mechi ya nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Benjamiani Mkapa kwa dakika 120.
Bao la Toky Rakotondraibe aliyemalizia pasi ya Randrianirina katika dakikaya 116 lilitosha kwa wapiga makasia hao kutinga fainali yao ya kwanza katika mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa ni ushirikiano wa Pamoja kwa mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda.

Madagascar ilianza kampeni yake kwenye kundi gumu lililokuwa na Tanzania (wenyeji), Burkina Faso, Mauritania na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Licha ya hali hiyo, chini ya uongozi wa Rakotondrabe, walipata pointi saba na kutinga robo fainali.
Kila mechi ilichezwa kwa mpango maalum ambao ni kushambulia kwa nguvu walipopata nafasi na kujilinda walipokabiliwa na mashambulizi.
Kocha huyo alisema: “Nguvu yetu ilikuwa mshikamano. Roho ya timu ilituvuta mbele. Tunao wachezaji wanaoweza kuleta tofauti, na sasa tunaamini katika nguvu ya kufanya kazi pamoja.”
Mshikamano huo umeonekana katika kila hatua kutoka kwenye mechi za makundi hadi kwenye ujasiri waliouonyesha dhidi ya Kenya kwenye hatua ya robo fainali.

Madagascar walipokutana na wenyeji Kenya mbele ya mashabiki elfu kadhaa Nairobi, walihitaji uvumilivu. Baada ya sare ya bao 1-1 kwa dakika 120, mchezo uliamuliwa kwa penalti. Hapo ndipo kipa mkongwe Michel Ramandimbisoa alipong’ara, akiokoa penalti muhimu na kuipeleka Madagascar nusu fainali kwa ushindi wa 4-3.
Kocha Rakotondrabe alikiri umuhimu wa ushindi huo: “Kuwashinda Kenya mbele ya mashabiki wao kulitupa nguvu kubwa. Tulitumia hilo kama motisha kwa ajili ya mechi yetu ya nusu.”
Kihesabu Madagascar imeonyesha kubadilika kulingana na wapinzani. Wamekuwa wakijibu vizuri mashambulizi wanapokutana na timu zinazoshambulia kwa kasi au zinazobana eneo.