Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimefungua shauri la maombi kuhusiana na uteuzi wa mgombea wake wa nafasi ya urais, Luhaga Mpina, baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumzuia kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali kuijaza.
Chama hicho kimefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dodoma, leo Jumatano, Agosti 27, 2025, kikiiomba mahakama hiyo iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea wao huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.
Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, Omar Issa Shaaban, amelieleza Mwananchi leo kuwa shauri hilo lililopewa usajili wa namba 21692 la mwaka 2025 limefunguliwa leo chini ya hati ya dharura sana, na limepangwa kusikilizwa kesho Alhamisi, Agosti 28, 2025.
“Tayari tumeshafungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma chini ya hati ya dharura sana, lililosajiliwa kwa namba 21692 la mwaka 2025 tumepangiwa kusikilizwa kesho na jopo la majaji watatu, Evaristo Longopa (kiongozi wa jopo), John Kahyoza na Abdi Kagomba,” amesema Shaaban.
Shauri hilo limefunguliwa na Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa ACT-Wazalendo na Luhaga Mpina, dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 umepangwa kufanyika Oktoba 29, 2025 na INEC inafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo wa vyama mbalimbali kwa watakaokidhi vigezo, leo Jumatano, Agosti 27, 2025, huku kampeni zikitarajiwa kuanza kesho Alhamisi, Agosti 28, 2025.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera yake katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, uteuzi wake huo ndani ya chama umebatilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.
Katika pingamizi hilo, Monalisa alidai kuwa uteuzi wa Mpina ndani ya chama hicho ni batili kwa kuwa hana sifa kutokana na kutokutimiza vigezo vya kikanuni, huku akirejea Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Chama, Toleo la mwaka 2015, kanuni namba 16(4) (i-iv).
Akirejea kanuni hizo, Monalisa alibainisha kuwa kanuni ya 16(4)(i) inaeleza kuwa mgombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, anapaswa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.
Kanuni ya 16(4) (iii) anapaswa awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
Kanuni ya 16(4)(iv) anapaswa awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.”
Monalisa katika pingamizi lake alibainisha kuwa Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho, Agosti 5, 2025 na alipitishwa na mkutano mkuu kupeperusha bendera yake Agosti 6, siku moja baada ya kujiunga na chama hicho.
Kufuatia pingamizi hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa katika uamuzi wake baada ya kusikiliza pande zote alikubaliana na hoja za pingamizi la Monalisa na kutengua uteuzi huo wa Mpina.
Kufuatia uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa, INEC nayo imemuondoa Mpina katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo katika uchaguzi huo.
Barua yake ya awali ya Agosti 15, 2025 (Kumb. Na. CBA.75/162/01A/229) iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi wa Kada huyo na kumzuia asijitokeze katika uteuzi unaoendelea leo jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa barua rasmi ya INEC, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Ramadhan Kailima, na kutumwa kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, INEC imefuta barua yake ya awali ya Agosti 15, 2025.
Sambamba na kufuta barua hiyo yenye kumbukumbu namba (Kumb. Na. CBA.75/162/01A/229) iliyomkabidhi Mpina inahusu urejeshaji wa fomu za uteuzi, pia INEC imemzuia Mpina kufika katika ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi uliopangwa kufanyika leo Jumatano, Agosti 27, 2025.
Licha ya kuelekezwa kuwa hatakiwi kufika katika ofisi ya tume hiyo leo, Mpina na ujumbe wake alikwenda katika ofisi hizo kwa lengo la kurejesha fomu yake ya uteuzi, lakini akazuiliwa na maofisa wa polisi kuingia ndani ya ofisi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Shaaban amesema chama hicho hakina mpango wa kuteua mgombea mwingine wa urais zaidi ya Mpina, na kwamba wanaamini uamuzi wa INEC ni batili kwani ni kinyume cha Katiba na Sheria.
Badala yake amesema kuwa wanachukua hatua za kisheria kwa kufungua shauri la maombi ya madai mahakamani kupinga uamuzi huo.
Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kwa njia ya simu, Wakili Shaaban amesema kuwa tayari wameshafungua shauri hilo na kwamba limepangwa kusikilizwa kesho Alhamisi.
Akizungumzia kuhusu kuchelewa uteuzi wa INEC ambao umefanyika leo, Shaaban amesema kuwa hakuna tatizo kwani uamuzi wa mahakama ukishatoka kama watakuwa wameshinda INEC italazimika kuutekeleza wakati wowote.