Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kuiboresha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ili kuwezesha Watanzania walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW, Prof. Mkenda alisema Serikali inajivunia mafanikio makubwa na hatua mbalimbali za Taasisi hiyo katika kushughulikia utolewaji wa elimu hiyo.
Mkenda ameitaka Taasisi hiyo katika kuadhimisha na kutafakari miaka 50 ya mafanikio kutafakari juu ya kuimarisha mifumo ya utoaji elimu bila ukomo kwa ikiwemo kufanya mapitio ya Sheria na Miongozo.
Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali itaendelea kusambaza miundombinu ya elimu nchini kote ambayo ni pamoja na kampasi za vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na shule ili kufanikisha upatikanaji wa elimu kwa wote.
Mkurugenzi wa TEWW, Prof. Philipo Sanga aliwasilisha mapendekezo manne ya kuboresha Tasisi hiyo, ikiwemo; kuandaa waraka maalumu kwa wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari waliokosa fursa ya kuendelea, ili waweze kupata elimu nje ya mfumo rasmi.
Kuweka Kituo Jumuishi cha Ujifunzaji Jamii katika kila kata, kwa ajili ya mafunzo mbalimbali yatakayoongeza ujuzi na maarifa kwa wananchi.
Prof. Sanga alisisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio hayo utaongeza ubunifu na kuhakikisha elimu inawafikia watu wengi zaidi, hususan waliokosa nafasi kwenye mfumo wa kawaida wa elimu.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Bw. Atupele Mwambene, alieleza kuwa TEWW imechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza adui ujinga nchini na kuwasaidia wananchi kupata maarifa ya kushughulikia changamoto za kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa shughuli za TEWW ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo inalenga kujenga mfumo wa elimu bila ukomo kwa kila Mtanzania.