Serikali yaonya wafugaji kuhusisha imani potofu kampeni chanjo ya mifugo

Chunya. Serikali Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya imeonya jamii ya wafugaji kuachana na dhana ya mila potofu kuhusishwa kwenye kampeni ya utoaji wa chanjo ya mifugo.

Hatua hiyo imetajwa kuchangia kukwamisha mikakati ya Serikali na  kuzorotesha ustawi wa mifugo na uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.

Katibu Tawala Halmashauri ya Wilaya  ya Chunya, Anakret Michombero amesema leo Jumanne Agosti  26, 2025 baada ya kuzindua kampeni ya  utoaji  wa chanzo  ya mifugo na uvalishaji heleni za utambuzi.

Amesema zaidi ya mifugo 170,000 wilayani  humo inatarajiwa kuchanjwa huku ng’ombe 200,000 tayari wamevishwa helena za utambuzi, lakini pia  asilimia 95 ya kitoweo cha kuku zimechanjwa.

“Kuna imani potofu miongoni mwa jamii kuwa wakichanja mifugo inakufa hiyo ni dhana potofu ya  vizazi na vizazi, lakini mnapaswa kutambua chanjo hiyo  ni muhimu kwa kulinda mifugo yenu ambayo ni faida kwa baadaye na familia zenu,” amesema.

Michombero amekemea dhana potofu na kuwasihi wafugaji kuchangamkia fursa ya  kuchanja mifugo ili kufikia malengo ya Serikali  na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ili kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo nchini.

“Kwa kutambua umuhimu wa chanjo na uvalishaji heleni Serikali imetenga siku maalum kwa ajili ya zoezi hilo ni vyema sasa jamii ya wafugaji maeneo ya pembezoni  kufikisha mifugo kwenye maeneo yaliyotengwa,” amesema.

Katika hatua nyingine  amewataka wafugaji kuisaidia  Serikali kutoa taarifa za siri za baadhi yao kuingia kinyemela bila kufuata utaratibu  na miongozo lengo ni kudhibiti  uvamizi wa maeneo ya malisho.

“Pia tutazuia mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayotokana na mwingiliano wa mifugo kutoka maeneo mengine nje ya Wilaya  ya Chunya,”amesema.

Ofisa Mifugo Wilaya ya Chunya, Dk Benedictor Matogo amewema wameweka mikakati  ya kufikia mifugo 170,000 katika kata zote Wilaya  ya Chunya baada ya kuzindua zoezi hilo.

Amesema mbali na kutoa chanjo na heleni tutaendelea  kutoa elimu kwa wafugaji kutumia mbinu bora za ufugaji. Pia malisho hususani unenepeshaji lengo ni kuleta tija kubwa katika sekta ya mifugo.

“Kimsingi tunamshukuru Serikali  kwa hatua hii kubwa, lakini kutufikishia vifaa vinavyo tumika katika kutoa  chanjo na uvishani wa heleni kwenye mifugo hususani  ng’ombe,” amesema.

Shija Mathias Mkazi wa Kijiji cha Mapula Wilaya ya Mbarali ameshauri Serikali kupitia  Wizara ya mifugo kuweka kipaumbele  kampeni hiyo kuwafikia jamii ya wafugaji  katika maeneo ya pembezoni.

“Tunatambua idadi kubwa ya mifugo ipo pembezoni, lakini pia kuangalia namna ya kudhibiti  uingizwaji holela kutoka mikoa mbalimbali nchini,” amesema.