Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa msimamo wake rasmi, ikifuta uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Kwa msingi huo, mamlaka hiyo imefuta barua yake ya awali ya Agosti 15, 2025 yenye kumbukumbu namba (Kumb. Na. CBA.75/162/01A/229) iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi wa Mpina na kueleza kuwa hatapaswa kufika katika ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi uliopangwa kufanyika leo Jumatano, Agosti 27, 2025.
Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Isihaka Mchinjita amekiri kupokea barua hiyo, akisema kwa hatua ya sasa inafanyiwa kazi mwanasheria wao.
“Tunamsubiri anakuja kutoka Zanzibar anaifanyia kazi na baadaye atazungumza na vyombo vya habari kwa hatua za awali, lakini pia viongozi wa chama tutakutana kujadiliana na kutoka na uamuzi unaofuata,” amesema Mchinjita.
Kwa mujibu wa barua rasmi ya INEC, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Ramadhan Kailima, na kutumwa kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, imeeleza uamuzi huo umechukuliwa baada ya taarifa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyobatilisha mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Agosti 6, 2025, ambao ulimteua Mpina kuwa mgombea urais.
Barua hiyo ya INEC, iliyoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, imeeleza;
“Napenda kukujulisha kwamba, tumepokea nakala ya barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ikieleza kuwa amebatilisha uamuzi wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo kwa sababu ya mgombea kukosa sifa za kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Vilevile, imetoa wito kwa ACT-Wazalendo kuteua mgombea mwingine mwenye sifa stahiki ili mchakato wa uteuzi uweze kuendelea kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi.
Hatua hiyo, imekuja huku chama hicho kikipanga kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, wakidai uamuzi huo ulikiuka taratibu za kisheria katika mchakato wa ndani wa chama wa kumpata mgombea urais.
Jana, Agosti 26, 2025 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa taarifa kwa umma, ikieleza kutengua uteuzi wa Mpina kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho.
Uamuzi huo, aliotoa baada ya ofisi hiyo kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliyelalamikia kupitishwa kwa Mpina, akidai kulivunja kanuni.
Mzizi wa yote hayo ni hatua ya Monalisa kukiandikia chama chake, kisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, akipinga uteuzi wa Mpina, kwa kurejea kifungu cha 16(4)i, iii na iv, cha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama toleo la mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kifungu cha 16(4)(i) “wagombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa. Awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.”
Aidha kifungu cha 16(4)(ii), kinasema wagombea urais/viongozi wa chama ngazi ya Taifa, “awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya mgombea wa chama.”
16(4)(iii) inasema, “awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
16(4)(iv) “awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.”
Katika barua yake, Monalisa alidai Mpina anakosa sifa zote hizo, kwani alijiunga na chama hicho, Agosti 5 na Agosti 6, mkutano mkuu ukampitisha kuwa mgombea urais.