WAKATI robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ikianza, ushindani umeongezeka tofauti na mechi za mwanzo wa msimu wa mashindano hayo.
Robo fainali ya BDL imezoeleka ushindani kuwa wa kawaida, lakini mwaka huu inavyochezwa ni vita na ni kama kombe liko uwanjani.
Ally Issa, kocha wa kikapu kutoka Morogoro anasema ushindani aliouona umetokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na timu zinazoshiriki ikizingatiwa kwamba hivi sasa kuna zawadi zinatolewa kila baada ya mchezo kwa wachezaji wanaong’ara katika mechi.
“Bila ya kufanya maandalizi ya kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa na kujituma katika mazoezi, robo fainali utaiona kuwa ni ngu-mu,” alisema Issa.

Katika mchezo wa robo fainali Stein Warriors iliifumua UDSM Outsiders kwa pointi 72-65, ambapo katika robo zote nne wababe walichomoza na ushindui.
UDSM ingeshinda kama ingetumia nafasi za kufunga katika robo ya kwanza ya dakika 2, 6 na pia robo ya pili katika dakika za 2, 6 na 9. Nafasi zingine iliyopoteza ilikuwa katika robo ya tatu dakika za 2, 4 na 6 na ile ya nne dakika ya 6 na 9. Katika mchezo huo mastaa wa Warriors walionyesha viwango bora wakiwafunika wenzao wa UDSM. Robo fainali hiyo inachezwa kwa timu kucheza michezo mitatu (best of three play off).
Nayo Pazi ilidhihirisha ubora kwa ushindi dhidi ya ABC wa pointi wa 63-50, ambapo iliingia uwanjani ikilenga kutwaa ushindii na pia kulipiza kisasi cha kufungwa katika mchezo wa kwanza kwa pointi 72-71.

TAUSI ROYALS VS DB TRONCATTI
Nguvu na akili iliyotumiwa na Tausi Royals dhidi ya DB Troncatti katika robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwa Wanawake (WBDL), iliifanya timu hiyo ishinde kwa pointi 68-60.
Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Donbosco Upanga, ambapo DB Troncatti iliyoingia uwanjani ikitumia mfumo wa kucheza mtu na mutu ilishindwa kuwadhibiti wachezaji wa Tausi Royals kutokana na kuzidiwa nguvu hasa nyakati za kutaka kupenya kwenda kufunga.
Katika mchezo huo, Juliana Sambwe wa Tausi Royals ndiye alikuwa mwiba kwa DB Troncatti kutokana asisti alizokuwa anatoa kwa wafungaji, huku Tukusubila Mwalusamba alikuwa kinara wa kupora mipira kwa wachezaji wapinzani wao na kwenda kufunga. Katika mchezo huo Tukusubila alifunga pointi 18 akifuatiwa na Juliana aliyefunga 13, ilhali upande wa DB Troncatti alikuwa ni Irene Gerwin aliyefunga 15 akifuatiwa na Jesca Lenga aliyetupia 12.
Tausi Royals itacheza na DB Troncatti katika robo fainali ya pili kesho na endapo Royals itashinda itaingia nusu fainali kwa ushindi wa michezo 2-0. Katika mchezo huo endapo DB Troncatti itashinda italazimu mchezo wa tatu uchezwe kuamua timu itakayocheza nusu fainali.

Kocha wa Vijana Queens, Kabiola Shomari alisema wanaendelea kutengeneza timu baada ya kuondokewa na wachezaji wao waliojiunga na timu zingine.
Shomari alieleza hayo baada ya timu yake kupoteza mchezo dhidi ya JKT Stars kwa pointi 52-36 katika robo fainali ya kwanza ya WBDL. Alisema baada ya kuondokewa na wachezaji hao waliwapandisha wachezaji kutoka katika kikosi cha pili cha timu yao maarufu kama City Queens.
Alitaja wachezaji hao kuwa ni Noela Uwendameno na Bhoke Juma (Jeshi Stars), Diana Mwendi, Tukusubira Mwalusamba, Tumaini Ndossi na Happy Danford waliotua Tausi Royals.