▪️Awataka wazingatie maadili, wadumishe uadilifu na kulinda usiri wa taarifa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watunza kumbukumbu wote nchini kuzingatia maadili ya kazi, kudumisha uadilifu na kulinda usiri wa taarifa zote zinazohifadhiwa kwani taarifa hizo ni nyenzo muhimu ya usalama wa Taifa na maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kinabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha nyaraka na kumbukumbu zote muhimu za Serikali pamoja na taasisi binafsi zinatunzwa kitaalamu na zinahifadhiwa.
Ametoa wito huo leo Jumatano (Agosti 27, 2025) wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
“Utunzaji sahihi wa nyaraka na kumbukumbu ni uti wa mgongo wa uwajibikaji, historia, na utawala bora. Bila masjala madhubuti, Taifa letu lingeweza kukabiliwa na changamoto kubwa za upotevu wa taarifa, ucheleweshaji wa maamuzi, na hatimaye kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa TRAMPA inapaswa kuendelea kuchochea uwajibikaji, utawala bora pamoja na kukuza utaalamu na weledi wa usimamizi wa nyaraka na kuhimiza utoaji wa mafunzo na miongozo ya kitaalamu ili kuhakikisha nyaraka zote zinatunzwa kwa viwango vya juu vya usiri, usahihi na usalama.
Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziagiza Taasisi zote za Umma ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Office zihakikishe zinaanza mara moja kutumia teknolojia hiyo ya kisasa kwani Serikali imewekeza katika mifumo hiyo kwa lengo la kupunguza matumizi ya karatasi, kuongeza kasi ya mawasiliano na kulinda siri za Serikali.
“Kupitia mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), Wizara, Idara, Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali zimewezeshwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa kumbukumbu, kuongeza uwazi na kupunguza ucheleweshaji wa huduma.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kulipa jumla ya shilingi bilioni 252.76 za malimbikizo ya mishahara ya watumishi 150,647 pamoja na kulipa shilingi bilioni 33.29 za malimbikizo ya mishahara ya wastaafu 10,022.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejiementi ya Utumishi wa Umma ma Utawala Bora, George Simbachanwene amesema kuwa Serikali imeeendelea kutoa ajira kwa watumishi wa umma wakiwamo watunza kumbukumbu. “Katika mwaka 2024-2025 kada hii tu ajira mpya zilizotolewa ni 965 waliopandishwa cheo ni 1,237, kuwabadilishia kada watumishi 59 (Recategorization) pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kiasi cha shilingi milioni 204.6”
Amesema kuwa Serikali inatambua mchango kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka katika ustawi wa utumishi wa umma na wakati wote itaendelea kutoa ushikiano kwa kada hiyo ili kuendelea kufanikisha masuala mbalimbali ya kiutumishi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman amepongeza wanachama wa chama hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya utunzaji wa siri za ofisi kwa maslahi ya Taifa. “Pamoja na hili ninawapongeza sana kwa uamuzi wenu mzuri wa ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa”.
Amesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa kada hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajenga jengo kubwa na la kisasa la utunzaji kumbukumbu ambalo litazinduliwa hivi karibuni. “Pia Serikali kwasasa inajenga majengo mapya ya kisasa na katika hili tunazingatia uwepo wa ofisi nzuri za watunza kumbukumbu.”
Awali, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota Mrope amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta mbalimbali iliwemo katika kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka.
“Rais Dkt. Samia amekuwa mwana TRAMPA namba moja, amepigania maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo sisi mwana TRAMPA, ametoa ajira nyingi katika kipindi kifupi ikiwemo kwa wanataaluma wa kada hii ya Menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka, amefanyia kazi changamoto zetu kwa kiasi kikubwa.”
Katika mkutano huo, TRAMPA wamemkabidhi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) ambayo wamesema yeye mwenyewe ataamua iende wapi kwa ajili ya matumizi kwenye sekta ya afya.