WMU YAJIIMARISHA KATIKA TATHMINI NA UFUATILIAJI.

……………

Na Sixmund Begashe -Dodoma 

Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) kupitia Kitengo  cha Ufuatiliaji na Tathmini, imewakutanisha wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka idara, vitengo na  taasisi zake kwa lengo la kujadili na kujipanga katika kutekeleza shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini wa Sera, Mipango, Mpango Mkakati, Ilani ya Uchaguzi (2025), miradi na programu mbalimbali za Wizara hiyo.

Akifungua kikao kakazi hicho Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Kitengo   cha Ufuatiliaji na Tathmini  Bi. Bure Nassibu , licha ya kuwapongeza wataalam hao kwa kazi nzuri wanazofanya, amesema kikao hicho ni muhimu katika kujipanga na kuhakikisha kuwa shughuli za Wizara zinafanyiwa ufuatiliaji na kupima utendaji kazi kila robo mwaka na kutoa taarifa na mapendekezo ya kuboresha Utendaji Kazi utakaowezesha kufikia malengo ya Wizara na Taifa kwa ujumla. 

Bi. Nassibu amewasisitizia wataalam hao, kukitumia kikao kazi  hicho vyema, katika kujijenga zaidi kwenye Ufuatiliaji na upimaji hali itakayochochea hari zaidi kwa watumishi kwenye utekelezaji wa majukumu yao kwa mwelekeo wa Dira ya Taifa (2050). 

Katika kikao kazi hicho,  washiriki walielezwa kuhusu umuhimu wa vikao vya kujadili utendaji kazi vya kila robo mwaka pamoja na kikao cha mapitio ya utendaji cha mwaka kitakachowajumuisha pia wadau wa Wizara kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wake.