Yanga yamaliza utata kuhusu Mzize

MABOSI wa Yanga umezima tetesi za mshambuliaji wa kikosi hicho, Clement Mzize kutimka kikosini humu kwa kuthibitisha kuwa ataendelea kuichezea timu hiyo hadi 2027.

Mzize alikuwa anatajwa kutua Esperance Sportive de Tunisia, pia alikuwa anahusishwa na Al Masry hivyo kwa mujibu wa Yanga nyota huyo ataendelea kusalia Jangwani.

Yanga imethibitisha hayo kupitia mtandao wao wa kijamii wakiweka wazi kuwa nyota huyo ataendelea kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili ijayo.

Mzize licha ya kwamba alikuwa akihusishwa kutakiwa na timu mbalimbali, lakini bado ana mkataba hadi 2027, hivyo tutakuwa naye msimu ujao 2025-2026 na 2026-2027 kwa mujibu wa mkataba alionao kwa sasa.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita 2024-2025 alifunga mabao 14 katika Ligi Kuu akiwa ndiye kinara wa klabu na nyota wengine wazawa katika ligi hiyo, amekuwa na mchango mkubwa eneo la ushambuliaji ndani ya Yanga imesema taarifa hiyo.

Akiwa tayari amecheza misimu mitatu tangu alipopandishwa timu ya wakubwa akitokea timu yetu ya vijana, Mzize amezidi kuwa mchezaji muhimu hadi timu ya Taifa Stars ambapo alifunga mabao mawili kwenye michuano ya CHAN 2024 inayoendelea kwa sasa.

Takwimu zinaonesha Mzize katika msimu wa kwanza 2022-2023 alikuwa sehemu ya kikosi

kilichotwaa taji la ligi kuu ya akifunga mabao matano na asisti moja.Kiwango chake cha kucheka na nyavu kimekuwa kikipanda msimu hadi msimu kwani 2023-2024 alifunga mabao sita na asisti saba.

Wakati msimu wa 2024-2025, Mzize amefunga mabao 14 na asisti sita, huku akicheza mechi zote 30 za msimu ulioisha, Mchango wa Mzize ndani ya Yanga upo wazi kwani kwa muda wote alioitumikia Yanga SC, kila msimu ameshinda ubingwa wa ligi, Kombe la Shirikiso michuano ambayo msimu wa 2023-2024 aliibuka mfungaji bora alipofunga mabao matano katika mechi sita, huku hat trick ikiwa moja.

Kubaki kwa mshambuliaji huyo kunaifanya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuwa na Prince Dube, Andy Boyeli na Edmund John aliyejiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars.