Dar es Salaam. Abiria wanaotumia usafiri wa daladala jijini Dar es Salaam, leo wamekuwa katika wakati mgumu baada ya usafiri huo kuwa adimu kutokana na daladala nyingi kukodiwa na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenda kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho.
Kampeni hizo za CCM zinafanyika leo Alhamisi Agosti 29,2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers ambapo wanachama ,wafusi na marafiki wa CCM watakutana huko.
Pamoja na mambo mengine katika uzinduzi wa leo mgombea wa urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan atahutubia akiwa sambamba na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 29,2025.

Ni kutokana na idadi kubwa ya watu kuelekea katika viwanja hivyo, Mwananchi imeshuhudia katika vituo mbalimbali vya daladala abiria wakihaha kutafuta usafiri.
Maeneo hayo ni pamoja na Chanika, Kigogo, Gongo la Mboto, Ukonga Banana hadi Tabata Segerea. Lakini hali hiyo pia ilionekana katika maeneo ya Mbagala Rangi tatu na viunga vyake, ambapo abiri wengi wamesimama vituoni huku daladala nyingi zikiwa zimebeba makada wa chama hicho waliovalia mavazi ya rangi za kijani na njano.
Kwenye vituo mbalimbali hasa vya pembezoni kumeonekana abiria wakikimbia huku na kule kujaribu bahati yao ya kupanda gari chache zinazosimama vituoni bila mafanikio kwani nyingi zimejaa.
“Leo nikifanikiwa kuingiza roho hata mwili ukibaki nje nitaona maana ninachelewa kazini na muda unazidi kwenda hakuna daladala sijui ni hawa wanaokwenda Kawe,”alisikika abiria akilalama katika kituo cha Tabata Segerea.
Kwa Chanika na Gongo la Mboto, daladala nyingi zinazobeba abiria kuanzia 40 ndizo zimekuwa adimu zaidi ambazo hizi husaidia kubeba watu wengi wanaokuwepo kituoni.
Kwa upande wa Segerea abiria walioonekana kuhenyeka zaidi ni wale wanaopanda gari za kwenda Kawe na Makumbusho, ambapo ilikuwa inapita hata dakika 20 gari hazijafika kituoni.

Aidha kwa gari zingine zinazofanya safari huko, zilikuwa zikibadilisha ruti kwa kile kilichoelezwa na madereva wake kwamba kuna foleni kubwa ambayo wakienda ni hasara.
“Kawe leo hakufai, kuna foleni kubwa sana, ndio maana nimeamua nibadili ruti niishie Buguruni ambapo ni pafupi unaenda na kurudi,”amesema Ramadhani Simba mmoja wa madereva wa daladala.
“Binafsi nitakwenda huko huko Kawe kwani tutabeba abiria kwa nauli nzuri sana leo,”amesema dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Kazungu, anayefanya safari kati ya Buguruni na Kawe.
Amefafanua kuwa licha ya kuwapo foleni atakwenda hata akipata ruti mbili zina faida kwani watu wengi wanaweza kuwatoza nauli wanayotaka.
“Hizi fursa haziji mara nyingi, tunaifuata hela hukohuko Kawe,”amesema huku anacheka.
Kwa upande wao abiria, Veronica Owiso mkazi wa Tabata Segerea, amesema amekaa zaidi ya nusu saa kituoni hajapata usafiri jambo lililomsababisha kuchelewa kwenda kufungua biashara yake.

Naye Charity Patrick, amesema imebidi kuunga magari ili kufika Kawe la sivyo alijiona namna atakavyochelewa kazini.
“Imebidi nipande gari tatu leo jambo ambalo sio kawaida, nimepanda la Segerea linalokwenda Tandika kisha nikashuka Tabata Mataa, pale nako za Kawe zikawa za taabu ikabidi nipande zinazoishia Mwenge zikitokea Mnazi Mmoja, halafu Mwenge ndio nikachukua la Kawe “amesema Charity.
Charles Kimath amesema leo imebidi atoboke mifuko kwa kuwa sehemu ya kwenda Sh600 na wakati mwingine Sh500 imebidi akodi bodaboda kwa Sh5,000 ili awahi kutokana na foleni iliyopo kuelekea Kawe.