Dar es Salaam. Baba mwenye umri wa miaka 63 (jina lake halijapatikana) mkazi wa Kijiji cha Sakwa Kusini kilichopo Kaunti ndogo ya Awendo nchini Kenya anadaiwa kumuua mwanaye wakati wakizozania chakula kisha kutokomea.
Tukio hilo limeripotiwa usiku wa Jumanne Agosti 26, 2025 baada ya marehemu mwenye umri wa miaka 28 kuripotiwa kwenda nyumbani kwa baba yake kudai chakula.
Inadaiwa kuwa baba huyo alikasirishwa na namna mwanawe alivyokuwa akitaka chakula ambapo walizozana vikali, hali iliyogeuka kuwa mauaji.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Awendo, Julius Kemboi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akishauri familia kutatua migogoro yao kwa njia bora na salama.
Katika tukio hilo Kamanda Kemboi amesema mzazi huyo alimpiga mwanaye huyo kwa jembe kichwani na kumsababishia majeraha mabaya na kufariki saa moja baada ya shambulio hilo.
“Tulipokea taarifa kutoka kwa majirani na tulipofika eneo la tukio, tulimkuta marehemu amelala kwenye dimbwi la damu. Alikuwa tayari amepoteza maisha kutokana na majeraha ya kichwa,” Kemboi ameiambia Tuko News.
Kwa mujibu wa majirani, kijana huyo wa miaka 28 hakuwa na uhusiano mzuri na familia, ambapo mara kwa mara walikuwa wakimtaka aoe ili aanzishe familia yake.
Mwili wa marehemu umepelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha Rosewood mjini Awendo, ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.
Kwa sasa maofisa wa Polisi wanaendelea na msako wa mzee huyo baada ya kutokomea kusikojulikana.