BI. OMOLO APONGEZA UKAMILISHWAJI WA JARIDA LA HAZINA YETU TOLEO LA NNE

Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (kushoto),
akikabidhiwa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Nne 2025, na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, Ofisini kwake
Treasury Square, Jijini Dodoma.

Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (katikati),
akiwa Katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Wizara ya Fedha, baada akikabidhiwa Jarida la Hazina Yetu Toleo la
Nne 2025, Ofisini kwake Treasury Square, Jijini Dodoma.

 

(Picha
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

……………………

Na
Josephine Majura WF, Dodoma
 

Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amekipongeza
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha Kwa kukamilisha Toleo la
Nne la Jarida la Hazina Yetu linalozalishwa na Wizara kupitia Kitengo hicho.
 

Bi.
Omolo ameyasema hayo Ofisini kwake Jijini Dodoma wakati wa kupokea Toleo la Nne
la Jarida hilo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, kwa niaba ya
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambalo huandaliwa na
Kitengo hicho kila baada ya miezi mitatu.
 

Alisema
kuwa Jarida hilo linamwonekano mzuri na makala pamoja na habari zake
zimepangiliwa vizuri.
 

“Natoa
rai kwamba muendelee kuhakikisha Jarida la “Hazina Yetu” linajikita kikamilifu
katika kuonesha majukumu ya msingi ya Wizara ya Fedha ikiwemo usimamizi wa sera
za fedha, ukusanyaji wa mapato ya Serikali, matumizi ya bajeti, na juhudi za
kukuza uchumi wa Taifa” alisema Bi. Omolo
 

Alisisitiza
kuwa Jarida hilo linapaswa kuendelea kuwa chombo cha kimkakati cha mawasiliano
ya Serikali, kinachowasilisha kwa uwazi na kwa lugha rahisi utekelezaji wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na mipango ya muda mfupi na mrefu ya Wizara.
 

Aidha,
alielekeza kuwa kila Toleo la Jarida liwe na muundo unaoakisi vipaumbele vya
Serikali, likijumuisha makala maalum kuhusu miradi ya kimkakati, mafanikio ya
kila robo mwaka, na changamoto zinazoshughulikiwa na Wizara.
 

 “Ni
muhimu sana kwa Kitengo chetu kuhakikisha taarifa hizi zinazotolewa zinawafikia
wananchi wengi zaidi na kwa wakati kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano
mlizonazo,” alisisitiza Bi. Omolo.
 

Akizungumzia
mabadiliko ya kidijitali, Bi. Omolo alieleza kuwa wananchi wa sasa wanategemea
kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, tovuti rasmi za Serikali, na
machapisho ya kidijitali, hivyo, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kiendelee
kutumia mikakati madhubuti ya kufikia makundi mbalimbali ya jamii kwa kutumia
majukwaa hayo kwa ufanisi.
 

Katika
hatua nyingine, Bi. Omolo alitoa pongezi kwa Kitengo hicho kwa juhudi
wanazozifanya katika kuhabarisha wananchi kuhusu majukumu na mafanikio ya
Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla.
 

Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Benny Mwaipaja,
aliahidi kuongeza juhudi na kuimarisha mbinu za mawasiliano ili kuhakikisha
wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu majukumu ya  Wizara.
 

Bw.
Mwaipaja alishukuru kwa pongezi zilizotolewa na Naibu Katibu Mkuu Bi. Jenifa
Christian Omolo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba
kwa Kitengo cha Mawasiliano nankwa uwezeshaji wa kufanikisha majukumu ya
Kitengo na kuahidi kuwa ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu
Mkuu yatatekelezwa kikamilifu na kutumika kama mwongozo wa kuboresha zaidi
Jarida la “Hazina Yetu” ili liendelee kukata kuu ya kihabari ya wadau wa
Wizara.

 MWISHO.