CAG AFANYA ZIARA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Hamis Dambaya, Ngorongoro.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu  za Serikali Bw. Charles Kichere  ametoa wito kwa watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na kushirikiana ili kulinda matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Akizungumza na menejimenti ya Ngorongoro, Kichere amesema njia pekee ya taasisi kufanya vizuri pale zinapokaguliwa ni kuzingatia sheria,Kanuni na taratibu zilizowekwa.

“Siku zote mnapotimiza majukumu yenu ya kila siku ni muhimu kuzingatia sheria, weledi na kukumbuka kuwa mpo ili kuwatumikia watanzania kupitia rasilimali mnazosimamia”,alisema bwana Kichere.

Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru alimpongeza CAG kwa ziara hiyo na kusema kuwa mamlaka itaendelea kuboresha mifumo utendaji kazi hususan kusimamia kikamilifu shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii ili kuendelea kuongeza tija kwa Taifa.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili kukagua shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo.