Jenerali Moses Ali anavyoutaka tena ubunge akiwa na miaka 86

Dar es Salaam. Madaraka matamu, ndiyo unavyoweza kusema baada ya Naibu Waziri Mkuu wa Pili na Mbunge wa Jimbo la Adjumani Magharibi mwa nchi ya Uganda, Jenerali Moses Ali (86), kusisitiza kuwa bado anautaka ubunge ili atumikie wananchi.

Kauli ya Jenerali Ali inakuja wakati ambao wakosoaji wamekuwa wakisema kuwa umri wake umeenda akimzidi hata Rais wa nchi hiyo Yoweri Museven , mwenye miaka 81. Jambo linalowafanya wengi kutia shaka ni umri wake mkubwa pamoja na hali yake ya afya.

Jenerali Moses Ali (86), ambaye licha ya hamu yake ya kuendelea kuongoza, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa watu wanaoamini kuwa amechoka na anatakiwa kupumzika ili kutoa nafasi kwa damu changa kuchukua uongozi, hatua ambayo imeendelea kuleta mvutano.

Hali hii inajiri wakati ambapo kambi yake imedharau wakosoaji wanaomtaka astaafu siasa za ushindani.

Ikumbukwe kuwa uteuzi wa wagombea wa Bunge, ikiwemo makundi maalumu nchini Uganda, umepangwa upya na sasa utafanyika Oktoba 15–16, 2025, katika ofisi za Wasimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya/Miji.

Maofisa wa kambi yake wamesisitiza kuwa Jenerali Ali bado ana uwezo wa kuchaguliwa tena bungeni ili kukamilisha miradi kadhaa aliyoianza na hajaikamilisha.

Tangu Juni 17, mwaka huu, alipoingia kwenye vichwa vya habari baada ya kuteuliwa kugombea akiwa ndani ya gari lake kushiriki kura za maoni za Chama cha National Resistance Movement (NRM) katika uchaguzi wa baadaye  Oktoba, mjadala mkubwa sasa ni kuhusu umri wake (miaka 86) na changamoto za kiafya. Wengi miongoni mwa wananchi wamekuwa wakihoji kwa nini bado anataka kuendelea na siasa, ilihali anamzidi umri hata Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni mwenye miaka 81.

Baada ya uteuzi, Jenerali Ali alianza kampeni za kutafuta kura, ikiwemo kufanya sherehe ya shukurani wiki iliyopita ambapo alijaribu kucheza ili kuonesha kuwa bado ana nguvu na afya yake ipo timamu.

Gabu Amacha, msaidizi wake wa kisiasa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni, amesema kinyume na mitazamo ya wananchi, bosi wake yupo imara na anatafuta kuchaguliwa tena ili kuwatumikia watu wa Adjumani.

“Yeye ndiye waziri aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uganda. Aliingia kwa mara ya kwanza serikalini mwaka 1973 kama Waziri wa Utawala wa Mikoa, baadaye akashika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Fedha; Vijana; Utamaduni na Michezo; Utalii, Wanyamapori na Mambo ya Kale; Biashara na Viwanda; Mambo ya Ndani; pamoja na Misaada, Maafa na Wakimbizi, miongoni mwa mengine,” amesema Amacha na kuongeza kuwa:

“Utumishi wake serikalini ulianza mwaka 1968 alipojiunga na Jeshi la Uganda kama ofisa mchanga na kupanda vyeo hadi kufikia hadhi ya Jenerali mwenye nyota nne.”

Amacha amepuuza hofu kuhusu afya ya Jenerali Ali, akisisitiza uzoefu wake wa muda mrefu kama mwanajeshi na mwanasiasa.

Miongoni mwa ahadi alizotoa iwapo atapewa ridhaa na wananchi ni pamoja na kuhakikisha Baraza la Mji wa Adjumani linapandishwa hadhi kuwa Manispaa, kuboresha miundombinu ikiwemo barabara na vituo vya afya, na kusimamia utekelezaji wa programu za Serikali.

Kati ya chaguzi za ubunge za mwaka 2001 hadi 2021, Jenerali Ali ameshinda zote isipokuwa ile ya mwaka 2006.

Kambi yake inasisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka 2026–2031 utakuwa wa mwisho kwake. Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa hajitokezi moja kwa moja majukwaani, badala yake huwakilishwa na timu ya kampeni au msaidizi wake wa kisiasa.

Kwa sasa wananchi wa Adjumani wamegawanyika kuhusu uamuzi wa Jenerali huyo wa miaka 86 kuwania tena tiketi ya NRM, ambapo anakabiliana na wagombea wengine wanne.

Mbio hizo zimeelezwa kuwa na ushindani mkali kati yake na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Nixon Owole. Wengine kwenye kinyang’anyiro ni Santos Adrawa na Moses Kibrai.

Abdul Amanya, mkazi wa Adjumani, amesema: “Ni wazi kuwa amekuwa msaada mkubwa kwa watu wa Kanda ya Madi. Uzoefu wake utasaidia sana kuendeleza maendeleo ya eneo letu.”

Hata hivyo, Margret Joan amesema: “Sasa amekuwa mzee, tungependa apumzike nyumbani kama shujaa badala ya kuendelea kujisumbua. Zaidi, Serikali inaweza kumpa nafasi ya kisiasa bila kulazimika kuwa Mbunge.”

Jenerali Moses Ali ni nani?

Jenerali Moses Ali, alizaliwa Aprili 5, 1939, ni miongoni mwa wanasiasa na wanajeshi wakongwe nchini Uganda. Alijiunga na jeshi akiwa kijana na alipata mafunzo ya juu nchini Israel na Uingereza, akipanda haraka kutoka Luteni Mshiriki mwaka 1969 hadi Brigedia mwaka 1974.

Alihudumu chini ya utawala wa Idi Amin kama Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye Waziri wa Fedha, kabla ya kuingia kwenye mgogoro na serikali hiyo na kupokonywa vyeo vya kijeshi.

Baada ya anguko la Amin mwaka 1979, Ali alikimbilia uhamishoni, kisha akaongoza kikundi cha waasi cha Uganda National Rescue Front (UNRF) katika miaka ya 1980.

Mwaka 1986 alisalimiana na Rais Yoweri Museveni na kuunganisha wapiganaji wake na jeshi la taifa, ambapo alipandishwa cheo hadi Meja Jenerali. Alipewa cheo cha Luteni Jenerali mwaka 2003 na Jenerali kamili mwaka 2012.