Kampeni ya CCM Kawe yaleta kicheko kwa wauza nyama choma, vyakula

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa chakula, vinywaji baridi, nyama choma, na vitafunwa katika viwanja vya Tanganyika Packers wameeleza kufurahishwa na mauzo mazuri kufuatia umati mkubwa wa watu  uliokusanyika kushuhudia uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wamefurika katika viwanja hivyo tangu saa 12 asubuhi ya leo Agosti 28,2025, wakiwa wamevalia mavazi ya rangi ya kijani na njano, rangi rasmi za Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuambatana na nyimbo na nderemo zilizoashiria hamasa ya kisiasa.

Wakizungumza kando mwa tukio hilo, baadhi ya wafanyabiashara wamesema shughuli hiyo imeongeza mzunguko wa fedha na kuwapa fursa ya kuuza bidhaa zao kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida.

“Leo biashara imeenza vizuri. Tumepata wateja wengi kuliko siku za kawaida kama unavyoona. Tunapongeza CCM kwa kuchagua eneo hili kufanyia uzinduzi,” amesema Selina Asha, muuzaji wa vitafunwa.

Amesema hadi sasa ameuza zaidi ya mara mbili ya ilivyo kawaida ya siku zote huku akimuomba Mungu mambo yazidi kuendelea vizuri.

Rehema Musa, muuza chai na maandazi, anaifananisha siku ya leo na Sikukuu ya Krismasi. “Watu ni wengi, na wengi wanahitaji chakula. Leo tu nimeuza zaidi ya mara tatu ya kawaida,” amesema kwa furaha.

Kwa upande wake, Juma Said anayeuza nyama choma na mishikaki, amesema tukio hilo si tu limemuongezea kipato, bali pia anaamini litampa motisha ya kuweka akiba kwa ajili ya kuendeleza biashara yake baada ya msimu wa kampeni.

“Ni muda mzuri wa kujipatia kipato cha haraka, lakini pia ni fursa ya kuwekeza katika biashara yangu ya baadaye,” amesema Juma.

Wafanyabiashara hao wametoa wito kwa Serikali na mamlaka husika kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa usalama na amani, wakati wa mikutano ya kampeni, wakisisitiza kuwa uchaguzi si wa vyama pekee, bali pia unatoa fursa ya kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo.

Uzinduzi huo wa kampeni za CCM, unaambata  na burudani mbalimbali, huduma za kijamii, pamoja na shughuli za kisiasa, hali iliyogeuza viwanja vya Tanganyika Packers kuwa kitovu cha shughuli na biashara kwa siku ya leo.

Katika mkutano huu, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi wanatarajiwa kutambulishwa kwa Watanzania kabla ya kuendelea na kampeni katika mikoa mbalimbali.

Wagombea hao ni miongoni mwa wagombea 17 walioteuliwa na INEC jana Agosti 27, 2025 kwa ajili ya kugombea urais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Wagombea hao na vyama vyao watakwenda kwa Watanzania kunadi sera zao ili wawapatie ridhaa ya kuongoza serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakati wakiwasubiri viongozi hao, vuguvugu la furaha linaendelea kushika kasi, wengi wao wakicheza na kuimba na kupiga tarumbeta sambamba na mirindimo ya nyimbo rasmi za chama hicho.