Kesi ya Mpina kuenguliwa urais yasikilizwa kwa njia ya mtandao

Dodoma. Kesi ya Luhaga Mpina wa ACT -Wazalendo dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) sasa inasikilizwa kwa njia ya mtandao.

Chama cha ACT-Wazalendo kimefungua shauri la maombi kuhusiana na uteuzi wa mgombea wake wa nafasi ya urais, Luhaga Mpina,  baada ya INEC kumzuia kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali kuijaza.

Shauri hilo limefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dodoma, jana Jumatano, Agosti 27, 2025, ambapo chama kimeiomba Mahakama hiyo iielekeze INEC kupokea fomu ya mgombea wao huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.

Mapema leo Agosti 28,2025 katika Mahakama Kuu Dodoma, Majaji walianzia kwenye kikao na Jaji Mkuu na baada ya kumaliza waandishi waliitwa na kuambiwa kuwa kesi itasikilizwa kwa njia ya mtandao.

Baada ya hapo kilitolewa kiunganishi kwa ajili ya kusikiliza mwenendo mzima wa kesi mbele ya majaji.