Mikoani. Ni kicheko na maumivu kwa wagombea wa nafasi ya ubunge na udiwani baada ya baadhi kuteuliwa na wengine kukosa sifa ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuanza safari ya kusaka kura kuwaongoza wananchi ngazi ya kata na jimbo.
Wagombea wa ubunge Jimbo la Moshi Vijijini kutoka chama Makini na Jimbo la Vunjo hawakurudisha fomu na wengine kwa ngazi ya udiwani wakikosa sifa ya kuteuliwa.
Uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa ubunge na udiwani kulingana na ratiba ya INEC ulianza Agosti 14 na kuhitimishwa Agosti 27.
Uteuzi wa wagombea wa ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani kwa Tanzania Bara unafanywa na wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika ngazi ya jimbo kwa wagombea ubunge na ngazi ya kata kwa wagombea udiwani.
Mkoani Mwanza, Jimbo la Ilemela wagombea 16 wa ngazi ya ubunge na wagombea 69 wa udiwani wameteuliwa kugombea nafasi hizo katika jimbo hilo mkoani hapo.
Msimamizi wa uchaguzi Ilemela, Herbert Bilia, leo Agosti 28, 2025, amesema kati ya wagombea 17 ambao walipatiwa fomu za uteuzi kwa ngazi ya ubunge, mgombea mmoja kutoka chama cha Ada-Tadea hakuteuliwa.
Hiyo ni kutokana na kuwa hadi saa 10 jioni ya Agosti 27, 2025 muda wa uteuzi kuisha, hakuwa amerejesha fomu hivyo kukosa sifa ya kuteuliwa.
“Ngazi ya udiwani, kati ya wagombea 81 waliochukua fomu, wagombea 12 hawakuteuliwa kutokana na mgombea mmoja kukosa wadhamini na wengine 11 hawakuteuliwa kutokana na kutokurejesha fomu hadi muda wa uteuzi unafika.”
Nako Moshi Mjini, msimamizi wa uchaguzi, Sifael Kulanga amesema wagombea wa vyama vya siasa 11 wameteuliwa kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Moshi Mjini.
Vyama hivyo vilivyoteuliwa ni CCM, Chauma, ACT-Wazalendo, CUF, Makini, SAU, CCK, NRA, TLP, AAFP, ADC.
Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo, Lucas Msele amesema wagombea kutoka vyama tisa ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), CUF, CCK, Ada-Tadea, TLP, NRA, ACT-Wazalendo na AAFP wameteuliwa kugombea ubunge.
“Jimbo la Vunjo pia wameteuliwa wagombea tisa kutoka vyama vya CCM, CHAUMMA, DP, ACT-Wazalendo, Ada-Tadea, Makini, CCK, AAFP na TLP,” amesema.
Msele amesema katika majimbo hayo mawili wagombea wawili ambao ni kutoka chama Makini Moshi Vijijini na NRA Vunjo hawakurudisha fomu.
Akizungumza, Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Siha, Marco Masue, amesema jumla ya wagombea sita wameteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo mwaka huu, ambapo wanatoka vyama vya CCM, ACT-Wazalendo, Makini, SAU, CUF na NRA.
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mwanga, Robert Tarimo, amesema wagombea watatu kutoka vyama vya CCM, ACT-Wazalendo na NRA wameteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo mwaka huu.
Amesema katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu walijitokeza wagombea kutoka vyama vitano, lakini mgombea wa NCCR-Mageuzi aliondolewa baada ya kukosa sifa za uteuzi kutokana na idadi ya wadhamini kutotimia, huku mgombea wa chama Makini hakurejesha fomu.
Nako mkoani Songwe, vyama vitatu vya upinzani vimefanikiwa wagombea wao kusimamisha wawakilishi kikiwemo chama cha Chaumma, CUF, ACT-Wazalendo na Makini.
Katika Jimbo la Tunduma, Chama cha ACT-Wazalendo kimemsimamisha Victor Mateni, Chama Makini kimemsimamisha Groly Mwaigomole na Chama cha CUF kimemsimamisha Kibona Balondeghe.
Kwa Jimbo la Ileje, INEC imewateua Raphael Fenihasi Kibona (CUF) na Mhandisi Godfrey Kasekenya Msongwe (CCM), na Jimbo la Vwawa ni Nkunyuntila Siwale (CUF), Onesmo Mnkondya (CCM) na Zambi Elia (ACT-Wazalendo).
Jimbo la Vwawa pia limewateua Japhet Hasunga (CCM), Happiness Kwilabya (Chaumma), Peter Kayuni (ACT-Wazalendo), Onesmo Kapungu (Makini) na Enock Mwaluka (CUF), huku Jimbo la Songwe, Philipo Mlugo (CCM) ameteuliwa.
Kwa upande wa Jimbo la Lupa Wilaya ya Chunya licha ya chama cha ACT- Wazalendo kumsimamisha mgombea lakini hadi muda wa kuhitimisha urejeshaji wa fomu ni mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM, Masache Kasaka ndiye kutangazwa mgombea pekee.
Msimamizi msaidizi wa Tume huru ya Uchaguzi Jimbo la Lupa, Athuman Bamba amemtangaza Masache Kasaka kuwa mgombea pekee katika jimbo hilo kwa kukidhi matakwa ya sheria ya Uchaguzi ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu.
Kwa upande wa Jimbo la Kyela kati ya wagombea watatu wa vyama vya upinzani walichukua fomu walio rejesha ni Baraka Mwamengo (CCM),Omary Mwakapaka (CUF ) huku mgombea wa Chama cha ACT – Wazalendo hakurejesha.
Jimbo Jipya la Uyole walio rejesha fomu ni Dk Tulia Ackson (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma ), Ipyana Samson, Chama cha Wananachi (CUF), Ibrahim Mwankwama na Chama cha ACT- Wazalendo, Wailes Mwalongo.
Kwa upande wa Jimbo la Mbarali, waliorejesha fomu ni Bahati Ndingo (CCM), Modestus Kirufi Chama cha ACT – Wazalendo.
Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani hapo, Rashid Athumani amesema chama hicho kilikuwa na wagombea saba waliochukua fomu INEC kugombea ubunge katika majimbo saba kati ya 11 ya Mkoa wa Morogoro, lakini wagombea watano tu ndio wamerudisha fomu hizo na kuteuliwa.
“Majimbo ambayo mpaka sasa wagombea wetu wamepata uteuzi ni pamoja na Kilosa, Ulanga, Malinyi, Morogoro Mjini na Morogoro Kusini Mashariki ambapo mgombea mmoja kutoka Jimbo la Kilombero hakurudisha fomu na majimbo mawili bado sijapata taarifa zake, nafuatilia na nitatoa taarifa zao jioni,” amesema Athumani.
Imeandikwa na Denis Sikonge (Songwe),Hawa Mathias (Mbeya) Saadar Amir (Mwanza),Florah Temba (Kilimanjaro) Hamida Sharif (Morogoro)