Dar es Salaam. Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameeleza kushangazwa na waliotaka Rais Samia Suluhu Hassan asigombee urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema mbona hawakufanya hivyo kwa wakuu wa nchi wa Serikali za awamu zilizopita.
Miongoni mwa wanaopinga hilo, amesema wapo waliomshushia lawama baada ya kushauri utaratibu wa kupitishwa kwa Rais Samia kuwa mgombea wa chama hicho, akieleza wanaofanya hivyo wanafanya kusudi au wanajitoa ufahamu.
Kauli ya Kikwete inajibu malalamiko ya baadhi ya wanachama wa chama hicho, akiwemo aliyekuwa Balozi wa Cuba, Humphrey Polepole aliyedai utaratibu uliotumika kumpitisha Rais Samia kugombea urais kwa CCM ulikiuka taratibu za chama hicho.
Polepole alikwenda mbali zaidi na kutaka, CCM iitishe upya mkutano mkuu na kumpitisha mgombea mwingine wa chama hicho, badala ya Rais Samia.
Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi Agosti 28, 2025 alipozungumza katika jukwaa la uzinduzi wa kampeni za urais za mgombea wa CCM, Rais Samia na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi.
Ameeleza inakuaje watu wapinge kupitishwa kwa kiongozi huyo sasa na hawakufanya hivyo kwa wagombea wengine wa urais katika awamu za Serikali zilizopita.
“Na mimi nililaumiwa kwa maneno niliyoyasema, na sasa nasema wanaoyasema hayo ama wanajisahaulisha au wanajitoa ufahamu. Utaratibu wanaujua na walikuwepo,” amesema.
Amesema tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi CCM imejiwekea utaratibu kwamba mkuu wa nchi aliyepo madarakani anapotaka kuendelea katika kipindi cha pili, anapewa nafasi.
Amesema imekuwa hivyo kuanzia kwa Rais wa kwanza hadi hayati John Magufuli, kwa nini iibuke mizengwe dhidi ya kupitishwa Samia.
“Mbona haya hatujayasikia kwa hayati Benjamin Mkapa, Kikwete wala Magufuli? kinachonishangaza hao wanaojifanya kimbelembele kuyasema haya wao nao walikuwepo,” amesema.
Ameeleza chama kilishajiwekea utaratibu wake na hapana budi uendelee na uheshimiwe.
Ameeleza mwangwi wa Samia mitano tena unaovuma sasa, umetokana na kazi iliyofanywa na mkuu huyo wa nchi.
Amesema mkuu huyo wa nchi amepokea nchi katika nyakati ngumu na watu walipata wasiwasi iwapo atamudu kuiongoza .
Ameeleza kauli ya Rais Samia kusema aliyesimama hapa ni Rais tena mwanamke ni uthibitisho kuwa, urais ni taasisi na haina jinsi.
“Naomba ikumbukwe kwamba marais sisi tuliopita kwenye huu mchakato wa tangu vyama vingi, tulikuwa na muda wa kujiandaa maana kila mmoja alijipanga na kutengeneza timu yake na watu wake na sera.
“Lakini, Samia alijikuta Rais ghafla bila kujiandaa amepata taarifa usiku wa manane. Alichukua muda mfupi kujiimarisha katika nafasi hiyo, alikuwa kama komando aliyetua kwa mwamvuli eneo la mapigano huku anapiga risasi,” amesema Kikwete.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose Migiro amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo ni ishara kwamba CCM imejiandaa vya kutosha kuanzia Dar es Salaam na maeneo mengine.
Ametoa hakikisho la kufanya kampeni za kistaarabu na kwamba, chama hicho kimedhamiria kuisaka dola.
Juma Issihaka, Aurea Simtowe, Peter Elias, Tuzo Mapunda, Devotha Kihwelo na Nasra Abdallah