Morogoro. Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na uharibifu mkubwa wa misitu unaochochewa na biashara ya kuni na mkaa. Nishati hii, inayotumika kwa wingi katika kupikia, husafirishwa kutoka Kilosa kwenda kuuzwa kwenye miji na majiji mbalimbali nchini.
Agosti 6 mwaka huu, mwandishi wa makala haya alizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, kuhusu hali hiyo na mikakati iliyowekwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Shaka alisema mkakati wa kwanza ni kuhakikisha misitu ya vijiji inalindwa na kuhifadhiwa, huku jamii zinazoiishi jirani zikipewa dhamana ya kuilinda.
Mkakati mwingine, alisema, ni kutafuta wadau watakaotoa elimu juu ya madhara ya nishati isiyo safi na salama, sambamba na kusambaza teknolojia za kisasa za kupikia ambazo zitapunguza matumizi ya kuni na mkaa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa jamii inapaswa kuondokana na mazoea ya kutumia kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi, rafiki kwa mazingira na salama kiafya.

Mfumo wa majiko ya gesi uliowekwa Shule ya Sekondari Morogoro kupikia chakula cha wanafunzi. Picha Hamida Shariff
“Hivi karibuni Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walikuja hapa Kilosa na kuleta majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo. Yaliuzwa kwa bei ambayo wananchi wanaweza kumudu na kwa kweli wengi waliyachangamkia,” alisema Shaka.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alisema kuna mradi wa usambazaji wa majiko banifu ulioanza Kilosa na baadaye utasambaa nchi nzima.
“Mradi huu unatekelezwa kwenye vijiji na miji. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi na salama kwa afya na mazingira,” alisema Mwijage.
Serikali imelipia asilimia 80 ya gharama za jiko, ambapo mwananchi hulipa Sh14,700 badala ya Sh73,500. Pia, kupitia mpango wa kusambaza majiko ya gesi na nishati safi kwenye taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100, REA imefikisha majiko ya gesi kwenye magereza yote nchini, na yote yameachana na kuni na mkaa, yakitumia gesi, makaa ya mawe na nishati nyingine salama.
Fatuma Ally, mama lishe na mkazi wa mtaa wa Behewa, alisema alihamasika kununua jiko hilo baada ya kuliona na kulijaribu kwa ndugu yake.
“Linaokoa mkaa. Kiasi kinachotumika kuiva chakula ni kidogo mno ukilinganisha na majiko tuliyoyazoea,” alisema Fatuma.
Alifurahia bei nafuu ya Sh14,700 na mfumo wa mauzo unaotumia kitambulisho cha NIDA, unaozuia mtu kununua jiko nyingi na kuuza kwa bei ya juu.
Fatuma alisema awali alitumia zaidi ya Sh100,000 kwa mkaa kila mwezi, lakini sasa anatarajia gharama kupungua kwa kuwa anatumia gesi na jiko banifu. Kabla ya kutumia gesi, alikuwa anatumia gunia mbili za mkaa kwa mwezi, lakini sasa matumizi yameshuka hadi Sh50,000.
Na baada ya kununua jiko hilo anatarajia kupunguza zaidi gharama.
Fatuma amesema kitu kingine alichopenda ni namna jiko hilo lilivyokuwa imara na pia namna Serikali inavyouza majiko haya kwa wananchi kwa kuzingatia utaratibu wa kitambulisho cha NIDA kwani inasaidia kudhibiti mtu kununua jiko zaidi ya moja na baadaye kwenda kuyauza kwa watu wengine kwa bei ya juu.
NCMC na WFP: Umeme shuleni, misitu kuokolewa
Mbali na mikakati hiyo, Wilaya ya Kilosa itanufaika na mradi wa pamoja wa National Carbon Monitoring Centre (NCMC) kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na World Food Programme (WFP) unaolenga kupunguza uharibifu wa misitu kwa kutoa nishati mbadala kwa shule na jamii.
Baada ya uhalisia kuwa asilimia kubwa ya kaya nchini na taasisi mbalimbali zinategemea matumizi ya kuni na mkaa huku maelfi ya hekta ya misitu yakikatwa kila mwaka, NCMC kwa kushirikiana na WFP, kimesaini makubaliano ya kutumia umeme kupikia katika shule 50 za msingi na sekondari.

Mtendaji Mkuu wa NCMC, Profesa Eliakim Zahabu, alisema mradi huu unatekelezwa Kigoma, Tabora, Dodoma na Dar es Salaam na baadae katika wilaya za mkoa wa Morogoro.
“Mradi huu utapunguza matumizi ya kuni na mkaa yanayochochea ukataji wa miti kwa ajili ya chakula cha wanafunzi,” alisema Zahabu.
Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Ronald Tran Ba Huy, alisema takribani hekta 500,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na matumizi ya kuni na mkaa. Moshi wa nishati hizo husababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya ndani, hususan kwa wanawake na watoto.
Habari hizi imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hizi, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917