Kocha Abdul Saleh amrithi Mngazija Uhamiaji FC

KIKOSI cha Uhamiaji FC kimemtambulisha Abdul Saleh Mohammed kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi ya Ali Bakar Mngazija.

Mngazija ambaye ametimkia Coastal Union ya Tanga, aliitumikia Uhamiaji FC kwa msimu mmoja pekee wa 2024-2025 ambapo timu hito ilimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Mbali na kufanya maboresho ya benchi la ufundi, pia timu hiyo imeachana na nyota wake wanne akiwemo Ali Mkadama, Daudi Kandidu, Daudi Goodluck na Masaoud Said ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu wa 2025-2026.

Wakati hayo yakijiri ndani ya Uhamiaji, Mlandege nayo imeachana na wachezaji saba akiwemo Mustafa Muhsin ‘Park’, AbdulNassir Makarani, Ally Njiwa, Khalfan Abdallah, Benson Young, Abdul Mahfoudh na Ally Kibweke.

Hadi sasa ikiwa dirisha la usajili kisiwani Zanzibar likiwa wazi, Chipukizi imeshika rekodi ya kufyeka wachezaji 10 ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao wa 2025-2026.