Maeneo 168 yaathiriwa mabadiliko tabianchi Zanzibar

Unguja. Jumla ya maeneo 168 ya fukwe, makazi na miundombinu ya barabara yameathirika na mabadiliko ya tabianchi kisiwani hapa, kati ya hayo 25 Unguja na 143 kutoka Pemba. 

Kutokana na athari  hizo, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Mazingira yenye kitengo maalumu cha mabadiliko ya tabianchi chenye jukumu la kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za mazingira na namna ya kukabiliana nazo ikiwa ni miongoni mwa hatua za kukabiliana na mabadiliko hayo.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Agosti 28, 2025 na Ofisa Mazingira kutoka kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar, Othman Bakar Burhan wakati wa ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. 

“Maeneo 168 yameathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi yakiwemo 25 Unguja na 143 Pemba, Fukwe, makazi na miundombinu ya barabara yote yameathiriwa. Hata hivyo  Serikali inaendelea kuchukua hatua za kurejesha maeneo haya katika uasili wake,” amesema Othman. 

Othman amesema zipo baadhi ya hatua zilizochukuliwa ikiwa pamoja na kupanda miti, kujenga matuta na kuta za mawe kando ya bahari ili maeneo hayo yasiendelee kuathirika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usafi na Mazingira Malindi, Mohamed Ibrahim Jidawi akionesha eneo lililofanywa jaa na wananchi ambalo lipo pembezoni mwa bahari.

Amesema, kujengwa kwa kuta pembezoni mwa bahari kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za kimazingira kwani mabadiliko hayo si tatizo la Zanzibar pekee, bali ni changamoto ya dunia.

Hivyo, amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, jamii na mashirika ya kiraia ni vyema kwa lengo kulinda mazingira na kuhifadhi historia ya visiwa vya Zanzibar kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usafi na Mazingira Malindi, Mohamed Ibrahim Jidawi amesema athari za mazingira zinachangiwa na tabia za kibinadamu kwa sababu baadhi yao wamegeuza fukwe kuwa jaa la takataka za majumbani.

Ameeleza, hali hiyo inasababisha taka kusukumwa kwenye makazi ya watu na kuhatarisha afya zao.

Naye,  Mwenyekiti wa Hifadhi ya Changuu Bawe (Chabamka), Abdallah Said Abdallah amesema fukwe ya Beitras zamani ilikuwa ikitumika kwa michezo na shughuli nyingine, lakini sasa haiwezi kutumika tena kutokana na athari za kimazingira.

“Baadhi ya wavuvi hutumbukiza mchanga baharini kwa ajili ya uvuvi, jambo linaloharibu mazingira ya bahari na kuchangia kina cha maji kupanda hivyo tunapaswa kuanzisha sheria itakayowabana wanaofanya vitendo hivi,” amesema Abdallah. 

Mkazi wa Kilimani, Wanu Makame Hassan amesema bado kuna uhitaji wa elimu kwa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Mamlaka husika zishuke kutoa elimu kwa wananchi na kujenga uelewa wa pamoja ili kuleta mafanikio ya kudumu katika vita dhidi ya mabadiliko hayo.”