Mahakama Kenya yazuia ujenzi wa kanisa Ikulu

Dar es Salaam. Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru kusitishwa kwa muda ujenzi wa kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika majengo ya Ikulu, nchini humo.

Agizo hilo la muda pia linazuia ujenzi kama huo katika Ikulu za Rais zilizoko maeneo mbalimbali nchini au hata jengo lolote lenye mafungamano na dini. Kwa mujibu wa tovuti ya Taifa Leo ya nchini humo. 

Hatua hiyo ni pigo kwa Rais William Ruto ambaye miezi ya karibuni alikaririwa hadharani akisema ameagiza kujengwa kwa kanisa la kudumu ndani ya Ikulu kwa fedha zake mwenyewe.

DW imeandika kwamba makundi manne ya kiraia yalipeleka pingamizi mahakamani kuzuia hatua hiyo yakisema ni kinyume cha sheria. 

Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu, imesema hatima ya ujenzi itasubiri uamuzi wa mwisho utakaotolewa Novemba, 2025.

“Agizo la muda linatolewa kuizuia Serikali ya Kenya, maofisa wake, au yeyote kwa niaba yao, kujenga kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika Ikulu ya Nairobi au katika Ikulu nyingine yoyote hadi Novemba 18, 2025,” amesema Jaji Chacha Mwita.

Zaidi ni kwamba agizo hilo lilitolewa kutokana na kesi iliyowasilishwa na mashirika manne ya kijamii Transparency International Kenya, Kenya Human Rights Commission, Inuka Kenya ni Sisi, na The Institute of Social Accountability yaliyopinga hatua ya Rais Ruto kuanzisha ujenzi wa kanisa ndani ya Ikulu ya Nairobi.

“Baada ya kuzingatia hoja za kesi na dharura ya jambo hili, ninaona kuwa ombi na kesi kuu zimeibua masuala muhimu ya kikatiba na kisheria yanayohusu uhusiano wa dini na serikali,” amesema.